Mshauri maalum ateuliwa kuchunguza kesi za Hunter Biden
12 Agosti 2023Katika taarifa yake iliyotolewa jana, Garland alisema kuna mazingira yasiyo ya kawaida kwenye suala hilo. Amemteuwa David Weiss ambaye tayari alikuwa anachunguza masuala ya kifedha ya Hunter Biden, baada ya makubaliano ya kukiri makosa kuvunjika. Mabadiliko haya ya matukio yamezusha maswali mapya kwenye kesi dhidi ya mtoto huyo wa rais wa sasa Marekani, zinazohusiana na ukwepaji kodi na kumiliki silaha, ambazo utatuzi wake ulikuwa karibu ufikiwe wiki chache zilizopita. Weiss mwenyewe, ambaye aliteuliwa kushika nafasi ya uwanasheria na rais wa wakati huo, Donald Trump, ndiye aliyeomba kuteuliwa kuwa mshauri maalum, kutokana na uzoefu mkubwa alionao kwenye uchunguzi dhidi ya Hunter Biden. Uchunguzi huu unakuja wakati Wizara ya Sheria ya Marekani ikiwa imechukuwa hatua zisizotarajiwa za kumshitaki Trump, hasimu mkubwa wa Biden kwenye uchaguzi uliopita na ujao, kwa kesi mbili za nyara za serikali na jaribio la kuzuwia matangazo ya uchaguzi.