1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, saa za Ulaya kubadilika kwa mara ya mwisho Jumapili?

27 Oktoba 2018

Saa za Umoja wa Ulaya zitarudi nyuma kwa saa moja siku ya Jumapili, yumkini kwa mara ya mwisho, lakini kuna hofu ya vurugu iwapo kila moja ya mataifa 28 wanachama litakwenda kivyake.

https://p.dw.com/p/37GgK
Zeitumstellung Sommerzeit
Picha: picture-alliance/dpa/S. Kahnert

Jumapili hii raia barani Ulaya wataweza kulala kwa saa moja zaidi na kufurahia mwangaza  zaidi nyakati za asubuhi katika kipindi cha miezi kadhaa ijayo. Lakini huenda ikawa mara ya mwisho kwa saa hizo kubadilika mwezi Oktoba kukaribisha majira ya baridi, na mwezi Machi kukaribisha majira ya machipuko.

Utaratibu huo umekuwepo kwa miongo kadhaa lakini suala la kukomesha kile kilichokuwa kikifahamika kama "daylight saving time" au wakati wa uokozi wa mwangaza wa mchana sasa lipo katika ajenda ya Umoja wa Ulaya.

Halmashauri kuu ya umoja huo ilipendekeza mwezi Septemba kusitisha mbadiliko hayo ya saa ya mara mbili kwa mwaka. Pendekezo la halmashauri hiyo linasema kila taifa mwanachama wa Umoja wa Ulaya linapaswa kusimamia muda wake lenyewe. Hu unaweza kuwa uamuzi wa mwisho utakaochukuliwa na halmashauri hiyo kuu na rais wake Jean-Claude Juncker, ambaye muda wake unamalizika mwaka ujao.

Jean-Claude Juncker EU Kommissionspräsident
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker akiangalia saa yake wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels. Juncker anataka kukamilisha suala la mabadiliko ya saa kabla ya uchaguzi wa bunge la Ulaya mwakani.Picha: picture-alliance/dpa/V. Mayo

Kura ya maoni ya Umoja wa Ulaya iliofanywa mitandaoni juu ya suala hilo ilibainisha kuwa asilimia 84  ya washiriki milioni 4.6 walipendelea kufutwa kwa mabadiliko hayo, ambapo asilimia kubwa zaidi walipendelea kubakisha saa za kiangazi. Idadi ya walioshiriki inaweza kuwa iliweka rekodi, lakini bado iliwakilisha chini ya asilimia moja ya idadi jumla ya watu katika kanda hiyo.

"Watu wanalitaka - tutalifanya hilo," alisema Juncker.

Lengo ni kuanza kutekeleza pendekezo hilo kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge la Ulaya katika msimu wa machipuko. Kufikia mwezi Aprili, nchi wanachama zitazingatia ni wakati gani zinazotaka kubakiza.

Kwa kuzingatia viwango vya Umoja wa Ulaya, hili litakuwa suala lililoamuliwa kwa haraka zaidi - sheria nyingi zinachukuwa miaka kuanza kutekelezwa.

Maswali bado yanasalia

Vikundi kazi vinavyotathmini athari za uamuzi huu, siyo tu kwa watu mmoja mmoja, lakini sekta nzima za biashara, kama vile usafiri wa treni na ndege, na wa usafirishaji bidhaa. Baadhi ya mataifa wanachama bado hayatangaza msimamo wao.

Estonia, Latvia na Lithuania, ambazo zipo mbele ya mataifamengi ya Umoja wa Ulaya kwa saa moja, zimependekeza muda wa kudumu wa msimu wa kiangazi. Slovakia  inataka muda wa kudumu wa majira ya baridi. Wakati huo huo Ureno inataka mfumo wa sasa uendelee wa kubadilisha saa mara mbili kwa mwaka.

Düsseldorf Zeitfeld
Uwanja wa saa ulioko katika bustani ya mji wa Dusseldorf katika jimbo la North-Rhine Westphalia.Picha: Imago/Future Image/C. Hardt

Kwa wakati huu kuna nyakati tatu tofauti, nchi 17 wanachama wa Umoja wa laya wanatumia saa moja katika eneo la Ulaya ya kati huku nchi nane za Mashariki kuanzia Filand na mataifa ya maeneo ya Baltic Kaskazini mwa Ugiriki na Cyprus upande wa Kusini yako mbele kwa saa moja.

EU yaelekea kuwa na mchanganyiko wa saa

Kwa sasa kuna zoni tatu za saa ndani ya Umoja wa Ulaya. Mataifa 17 wanachama yanatumia muda wa saa za Ulaya ya Kati (CET), na toleo lake la majira ya kiangazi, CEST. Mataifa manane, kuanzia Finland na mataifa ya Baltic upande wa kaskazini kuelekea Ugiriki na Cyprus upande wa kusini, yako saa moja mbele.

Mataifa matatu, Ureno,  Uingereza na Ireland yako saa moja nyuma. Austria, ambayo kwa sasa inashikilia urais wa kupokezana  wa Umoja wa Ulaya inalenga kuzuwia mkanganyiko. Imeibuka kuwa mtetezi wa muda wa kudumu wa msimu wa kiangazi, lakini nia mjini Vienna ni kukubaliana juu zoni moja ya muda katika kanda ya Ulaya ya Kati.

Mataifa ya Benelux - Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg - pia yana mpango wa kushauriana. Ujerumani, taifa kubwa kabisaa ndani ya Umoja wa Ulaya kwa vipimo vingi zaidi, inaelemea zaidi muda wa kudumu wa msimu wa kiangazi. Suala hilo linatarajiwa kuibuliwa wakati wa mkutano wa faragha wa mawaziri wa usafiri wa Umoja wa Ulaya mjini Graz, Austria, wiki ijayo.

Je, zoni tofauti za muda litakuwa tatizo?

Shirika la reli linalomilikiwa na serikali ya Ujerumani, Deutsche Bahn halina wasiwasi kuhusu huduma zake za kimataifa. Saa za mataifa jirani zitapaswa kutajwa tu kama "saa za mahali pale", alisema msemaji wa shirika hilo mjini Berlin. Hii tayari ndiyo hali kwa huduma za shirika hilo kwenda mjini Moscow.

Schlaflosigkeit
Mwanaume akiwa amelala kitandani mjini Hamburg, Ujerumani na kutazama saa yake ya mezani. Baadhi ya watu wamehoji kuwa mabadiliko ya saa yana madhara ya kiafya.Picha: picture-alliance/dpa/C. Klose

Sekta ya usafiri wa ndege haijaonyesha kupenda, ikiamini kwamba ratiba za kimataifa ambazo tayari ni ngumu zitazidi kuwa ngumu. Jambo moja ni kwamba safari za ndege zinaweza kunaza kwa kuchelewa zaidi katika majira ya baridi, na matokeo yake yakawa kusogea katika marufuku za safari za usiku kwenye viwanja vingi.

Pendekezo la Halmashauri kuu linao uungwaji mkono katika bunge la Ulaya, ambako kuna miito ya kuchukuliwa uamuzi wa haraka kuhusu kubadili mfumo huu ambao umekuwepo katika Umoja wa Ulaya tangu 1996. Mwaka huo, mataifa yote wanachama yalikubali kubadilisha saa zao katika mtindo sawa mwezi Machi na Oktoba.

Lengo lilikuwa kuokoa mwangaza wa mchama na nishati, lakini faida zake zina utata, huku kukiw ana wasiwasi kuhusu madhara ya kiafya.

"Kama tusingelikuwa na mabadiliko haya, na baadhi ya watu wakaja na wazo ya kuyaanzisha, kila moja angesema walikuwa na kichaa," anasema Peter Liese, msemaji wa kamati ya afya wa kundi la wabunge wa kihafidhina katika bunge la Ulaya, EPP.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga