Frauen-WM
18 Julai 2011Michuano ya fainali za kombe la dunia upande wa wanawake, kwa mtazamo wa Ujerumani, haikuwa "maajabu ya msimu wa kiangazi" kwasababu "binti mfalme" aliondolewa kabla ya wakati. Kwa jumla, lakini, michuano hiyo, bila ya shaka yoyote, ilifana. Viwanja vilijaa pomoni.
Mashabiki walishangiria michuano ya fainali za kombe la dunia mfano wa sherehe za familia. Kabumbu la wanaume halina tena cha kujivunia. Warembo wamefanikiwa wakati wote wa michuano hiyo kulisakata dimba, sio tu la kusisimua, bali pia la kuvutia, kiufundi na ustadi wa hali ya juu.
Mtu hajakawia kugundua kwamba ulimwengu unazidi kujongeleana katika soka la wakinamama. Naiwe Guinea ya Ikweta, Columbia au New Zealand, hata mataifa madogo ambayo yalilazimika kufunga virago baada ya duru ya kwanza kumalizika, yalionyesha na wao ujuzi walio nao.
Na jambo hilo limechangia pakubwa katika kuyapatia sura ya kuvutia mashindano hayo. Kati ya wale waliokuwa wakipigiwa upatu kuwa na nafasi nzuri ya kuwika, baadhi walitimuliwa mapema kuliko ilivyotegemewa. Robo fainali zilikuwa kituo cha mwisho kwa Uengereza, Brazil na Ujerumani pia.
Hata katika soka la warembo, uwezo wa wastani hautoshi kuifanya timu isonge mbele.
Timu ya Ujerumani imejikwaa zaidi kutokana na matarajio makubwa iliyowekewa. Jamii iliamini hakuna shaka yoyote timu ya kocha Silvia Neid ingevikwa kwa mara ya tatu mfululizo taji la mabingwa wa dunia kwa kua mcheza kwao hutunzwa. Lakini mithali hiyo ilishindwa maji yalipozidi unga.
Katika duru ya kwanza tuu walipoteremka uwanjani dhidi ya Ufaransa ndipo warembo wa Ujerumani -"Die Mannschaft"- walipoonyesha ujuzi wao wa kweli. Kocha wa timu ya taifa, Silvia Neid, alilazimika kumeza machungu.
Lakini uamuzi wake uliobishwa wa kutomteremsha uwanjani Birgit Prinz, ulikuwa sawa. Mshindi huyo wa dunia kwa mara tatu na mchezaji nyota aliyeweka rikodi katika daraja ya taifa hakuwa katika hali yake ya kawaida, kimchezo.
Lakini angalao mwishoe watu wameweza kupangusa machozi. Ujerumani ilitolewa na timu iliyokuja tawazwa mabingwa wa dunia. Wajapani wamestahiki kuvikwa taji hilo. Kimchezo walikuwa na nguvu, mastadi, nidhamu na walijiotokeza kuwa wamoja.
Ndio maana baadae tumeshuhudia "maajabu ya msimu wa kiangazi". Kwa Japan ambayo baada ya Tsunami na balaa la mionzi ya kinuklea msimu wa mapambazuko mwaka jana, angalao imefarijika japo kidogo kwa kuibuka na ushindi wa kombe la dunia la wakinamama.
Mwandishi: Nestler Stefan/ZPR/Hamidou Oummilkhheir
Mhariri: Miraji Othman