1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yashambulia vikali Hezbollah mjini Beirut

6 Oktoba 2024

Maafisa wa Mamlaka ya Wapalestina wamesema shambulizi la angani la Israel mapema siku ya Jumapili, dhidi ya msikiti mmoja katika Ukanda wa Gaza, limeua watu 19.

https://p.dw.com/p/4lSV1
Lebanon | Mashambulizi ya anga ya Israel huko Beirut
Mashambulizi makali na milipuko mikubwa yasikika Beirut na viunga vyakePicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Shambulizi la Israel lilipiga Msikiti huko Gaza ambalo lilikuwa likiwahifadhi wakimbizi wa vita, karibu na hospitali kuu katikati ya mji wa Deir al-Balah.

Israel ilisema bila kutoa ushahidi kwamba ililenga kamandi ya Hamas na kituo cha udhibiti cha wanamgambo hao vilivyoko katikati ya maeneo ya raia.

Jeshi la Israel limetangaza operesheni mpya ya ardhini na angani eneo la Jabaliya, kaskazini mwa Gaza. Eneo hilo lina kambi inayowahifadhi wakimbizi wengi wa vita vya tangu 1948.

Unaweza pia kusoma: Zaidi ya watu nusu milioni wamekimbia makazi yao Lebanon

Israel, imezidisha mashambulizi kaskazini mwa Gaza na kusini mwa Beirut, katika vita vyake vinavyoendelea kutanuka katika ukanda wa Mashariki ya Kati, dhidi ya makundi ya wanamgambo yanayoungwa mkono na Iran.

Nchi hiyo ingali inapambana na wanamgambo wa Hamas ndani ya Gaza, ikiwa ni mwaka mmoja tangu shambulizi la Oktoba 7, 2023. Mzozo huo umechochea makabiliano mengine ya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon.

Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na Ujerumani ni miongoni mwa nchi ambazo zimeorodhesha Hamas na Hezbollah kuwa makundi ya kigaidi.

Israel yatoa agizo jipya kwa wakaazi wa Gaza Kaskazini kuondoka

Jeshi hili lilisambaza picha na video kuonyesha vifaru vyake vya kivita vikielekea eneo hilo.

Mzozo kati ya Israel na Hezbollah wapamba moto

Limeongeza kuwa vikosi vyake vimelizingira eneo la Jabaliya, huku ndege zake za kivita zikishambulia ngome za wanamgambo kuelekea operesheni hiyo kamili.

Unaweza kusoma pia: Israel yasema wanamgambo 15 wameuwawa Lebanon

Hapo nyuma, Israel imefanya operesheni kadhaa katika eneo hilo, lakini baadaye makundi ya wanamgambo huibuka tena.

Israel pia imetoa amri mpya ya kuwataka wakaazi wa kaskazini mwa Gaza kuondoka. Jeshi la Israel limesema "Tuko katika awamu mpya ya vita”.

Kulingana na msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee, jeshi la Israel limetanua eneo linaloitwa la shughuli za kibinadamu kusini mwa Gaza, na kuhimiza watu kuelekea huko.

Ukanda huo unajumuisha kambi za mahema zilizoenea ambapo mamia ya maelfu ya watu tayari wametafuta hifadhi, na Israel imefanya mashambulizi ndani yake dhidi ya wale inaowataja kuwa wapiganaji wanaojificha miongoni mwa raia.

Unaweza pia kusoma: Hofu yatanda Mashariki ya Kati baada ya mashambulizi ya Iran

Kule kusini mwa Beirut nchini Lebanon, mashambulizi makubwa ya angani na miripuko mikubwa imesikika ndani na viunga vya mji wa Dahiye, usiku kucha wa kuamkia Jumapili.

Israel yashambulia katikati mwa Beirut

Israel yasema mashambulizi yamelenga vituo vya wanamgambo wa Hezbollah.

Miongoni mwa maeneo yaliyoshambuliwa ni pamoja na jengo lililoko mkabala na barabara kuelekea uwanja pekee wa kimataifa wa ndege nchini Lebanon, na jengo jingine linalotumiwa na chombo cha utangazaji Habari Al-Manar, kinachomilikiwa na Hezbollah.

Jeshi la Israel, IDF limethibitisha kufanya mashambulizi hayo karibu na Beirut. Aidha, IDF limesema pia kwamba takriban makombora 30 yalifyatuliwa kutoka Lebanon kuelekea Israel, na baadhi yalidunguliwa.

Unaweza pia kusoma: Israel yamuua kamanda mwingine wa Hezbollah

Kundi la Hezbollah limesema lilifanikiwa kulenga kundi la wanajeshi wa IDF kaskazini mwa Israel na kuwashambulia kwa makombora. Vyombo huru havikuweza kuthibitisha madai hayo.

Inaripotiwa kuwa Walebanon wasiopungua 1,400, wakiwemo wahudumu wa afya na wanamgambo wa Hezbollah wameuawa na watu milioni 1.2 wamelazimika kuyakimbia makwao chini ya majuma mawili yaliyopita.

Israel imesema lengo lake ni kulitimua kundi la Hezbollah kutoka mpaka wake ili makumi ya maelfu ya raia wa Israel waweze kurudi katika makaazi yao kwenye eneo hilo.

Fahamu mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel na Hamas.

Chanzo: APE