Hofu yatanda Mashariki ya Kati baada ya mashambulizi ya Iran
2 Oktoba 2024Usiku wa kuamkia Jumatano, Iran ilivurumisha makombora ya masafa marefu yapatayo 180 kuelekea Israel ikisema ilikuwa ikiyalenga maeneo na miundombinu ya kijeshi. Hata hivyo, Israel imesema asilimia kubwa ya makombora hayo yalinaswa na kuharibiwa na mfumo wa ulinzi wa anga kwa kusaidiwa na washirika wake kama Marekani, Uingereza na Ufaransa.
Lakini Tehran imesisitiza kuwa makombora yake mengi yalilenga shabaha zao huku Mohammad Bagheri, mkuu wa majeshi wa Iran akiionya Israel kuwa isipojizuia, operesheni hiyo ya jana usiku inaweza kujirudia.
"Iwapo utawala wa Kizayuni ambao umeingiwa wazimu na usipodhibitiwa na Marekani na Ulaya, na unataka kuendeleza uhalifu huu au kuchukua hatua dhidi ya uhuru wa taifa letu, operesheni ya usiku wa jana itarudiwa kwa nguvu kubwa na miundombinu yote ya serikali ya Israel italengwa."
Soma pia: Iran yaishambulia Israel kwa makombora 180
Hadi sasa hakuna taarifa zozote kuhusu majeruhi kufuatia mashambulizi hayo. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Iran imefanya kosa kubwa kuishambulia nchi yake na kuapa kulipiza kisasi.
Rais wa Marekani, Joe Biden amesema nchi yake inaiunga mkono kikamilifu Israel na kuwa kuna mazungumzo yanayoendelea kuhusu jinsi Israel itakavyojibu shambulizi la Iran huku akisisitiza kuwa athari kwa serikali ya mjini Tehran zitaonekana.
Miito ya kimataifa ya kutouchochea mzozo huo
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amelaani mashambulizi ya Iran na kusema yanahatarisha kulitumbukiza eneo zima katika vita. Kwa upande wake Urusi imetoa wito wa kutouchochea mzozo huo, lakini ikaikosoa Marekani na kusema kuwa sera na diplomasia yake katika eneo la Mashariki ya Kati imeshindwa kabisa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha mkutano wa dharura leo Jumatano ili kuujadili mzozo wa Mashariki ya Kati unaoendelea na ambao umesababisha mparaganyiko wa safari za ndege kutokana na kitisho cha usalama. Iran imetangaza kuifunga anga yake kufuatia kitisho cha mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel.
Wakati hayo yakiendelea, vijana wawili wakazi wa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu waliwaua hapo jana watu saba na kuwajeruhi wengine 17 katika shambulio la risasi na visu mjini Tel Aviv. Pia, milipuko miwili ilitokea karibu na ubalozi wa Israel mjini Copenhagen nchini Denmark huku ubalozi mwingine wa Israel nchini Sweden ukishambuliwa kwa risasi.
Hayo yakiripotiwa, Israel imeanzisha operesheni ya ardhini dhidi ya kundi la Hezbollah nchini Lebanon na kuwaamuru raia wa vijiji 24 kuondoka. Makabiliano ya ardhini yameripotiwa kusini mwa Lebanon katika mji wa Adaisseh. Mataifa mbalimbali yameendela kuwaondoa raia wao nchini Lebanon.
Vyanzo: (DPAE, AP, Reuters, AFP)