Israel yashambulia Syria
31 Januari 2013Nabil al-Arabi mkuu wa Jumuiya ya nchi za kiarabu amesema ukimya wa jumuiya ya kimataifa juu ya mashambulizi ya hapo nyuma ya Israel nchini Syria ndio ulioipa nguvu nchi hiyo kufanya shambulizi jengine kufuatia hali ya kiusalama na ya kisiasa nchini Syria inayozidi kudorora.
Wakati huo huo Urusi imeonesha wasi wasi wake juu ya shambulizi la Israel katika taasisi ya utafiti ya kijeshi nchini Syria, ikisema kuwa shambulizi kama hilo kamwe halikubaliki. Kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Urusi, shambulizi hilo litakapothibitishwa, Israel itakuwa imekiuka kwa kiwango kikubwa mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Hapo jana serikali ya Syria ilitangaza kuwa ndege za kijeshi za Israel zililenga taasisi yake ya utafiti wa kijeshi kaskazini magharibi mwa mji mkuu, Damascus. Watu wawili waliuwawa na wengine watano wamejeruhiwa katika shambulizi hilo. Hata hivyo Syria ilikanusha ripoti kuwa Israel ililenga msafara wa magari yaliyokuwa na silaha za kivita karibu na mpaka wa Lebanon.
Israel haijatoa tamko rasmi juu ya shambulizi
Hadi sasa hakuna tamko lolote rasmi juu ya tukio hilo kutoka kwa serikali ya Israel. Nchi hiyo mara kwa mara imekuwa na hofu kwamba silaha mbali mbali zimekuwa zikisafirishwa kutoka Urusi hadi Syria na kwamba huenda silaha hizo zikaangukia mikononi mwa kundi la Hezbolla ambalo ni washirika wa Syria.
Hezbollah kwa upande wake imelaani shambulizi la Israel na kusema ni hatua ya nchi hiyo kuiharibu Syria.
Israel ilinukuliwa na vyombo vya habari nchini humo ikisema haitakubali silaha zozote zinazotoka Iran, Korea kaskazini, na Urusi kufikia makundi ya kigaidi kama Hezbollah ambayo ni washirika wakubwa wa Syria, Iran. Hii ni kulingana na Tzahi HaNegbi ambaye ni mbunge kutoka chama cha Likud anayejulikana kuwa karibu sana na waziri mkuu Benjamin Netanyahu.
Kando na hilo Urusi imekuwa ikikosolewa na jamii ya Kimataifa pamoja na Jumuiya ya nchi za kiarabu kwa kukataa kujiunga na wito wa kimataifa wa kumtaka rais Bashar al Assad kuondoka madarakani ili kukomesha umwagikaji wa damu unaoendelea kwa miezi 22 sasa tangu kutokea kwa maandamano ya kutaka mabadiliko nchini humo.
Urusi inasemekana kuwa bado inaendelea kupeleka silaha nchini Syria. Takriban watu 60,000 wameuwawa tangu kuanza kwa ghasia hizo mwezi machi mwaka wa 2011.
Mwandishi Amina Abubakar/dpa/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba