1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban awasihi wapiganaji Syria kuheshimu utu

Admin.WagnerD30 Januari 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa wito kwa wapiganaji wote katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria kuacha mapigano kwa ajili ya kuthamini ubinaadamu.

https://p.dw.com/p/17Txq
Katibu Mkuu Ban Ki-moon.
Katibu Mkuu Ban Ki-moon.Picha: AFP/Getty Images

Ban ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kukusanya fedha kiasi bilioni 1.5 kwa ajili ya wakimbizi wasyria, unaofanyika nchini Kuwait. Amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa zaidi ya wasyria milioni 4 wanahitaji msaada wa dharura,na kwamba raia wa kawaida wanateseka kupita kiasi, hivyo wanahitaji kupatiwa msaada sahihi. Umoja wa Mataifa unapanga kuwapatia mahitaji ya msingi raia milioni 4 waliyoko ndani ya Syria, na zaidi ya wakimbizi 650,000 waliyoyakimbia makaazi yao kutokana na mgogoro huo unaokaribia miaka miwili.

Mfalme wa Kuwait, Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah.
Mfalme wa Kuwait, Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah.Picha: Getty Images

Kuwait yatoa dola milioni 300

Wawakilishi kutoka mataifa zaidi ya 60 wanahudhuria mkutano huo wa kimataifa kusikia maombi ya Umoja wa Mataifa ya kuchangisha dola bilioni 1.5. Maafisa wa umoja huo wanasema wana kiasi kidogo tu cha fedha zinazohitajika, ingawa ahadi kutoka mataifa na mashirika mbalimbali ziliongezeka kabla ya kuanza kwa mkutano huo. Umoja wa Ulaya na marekani ziliahidi kutoa jumla ya dola milioni 400.

Mfalme wa Kuwait Sheikh Sabah al-Ahmad al-Saba, naye ametangaza leo kuwa atachangia dola milioni 300. Sheikh al-Saba ameuambia mkutano huo kuwa taarifa za kutisha juu ya vurugu zinazoendelea nchini Syria,zinazua maswal ijuu ya mustakabali wa Syria, na kuongeza kuwa juhudi za msaada zinapaswa kuongezwa mara mbili. Umoja wa Falmeza Kiarabu nao ulitarajiwa kutoa kiasi cha dolamilioni 300.

Brahimi alitaka baraza la usalama kuchukua hatua sasa

Mjumbe wa kimataifa wa amani katika mgogoro wa Syria, Lakhdar Brahimi alisema vita nchini Syria vimefikia kiwango cha kutisha ambacho hakijawahi kushuhudiwa, baada ya wanaume kadhaa kukutwa wakiwa wamechinjwa. Brahimi aliliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumanne, kuwa linapaswa kuchukua hatua sasa hivi kukomesha mauaji ya kutisha, kama yanayoshuhudiwa hivi sasa ikiwa ni pamoja na yale ya wanaume wasiyopungua 78, kilamoja wao akiwa ameuawa kwa kupigwa risasi moja na kisha kutupwa mtoni katika mji wa Aleppo.

Mama akimshika mtoto wake aliyejeruhiwa akisubiri matibabu katika hospitali nchini Syria.
Mama akimshika mtoto wake aliyejeruhiwa akisubiri matibabu katika hospitali nchini Syria.Picha: Z.Baillie/AFP/Getty Images

Baada ya miezi 22 tangu kuanza kwa mgogoro huo, watu zaidi ya elfu 60 wameuawa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.Brahimi alisema uhalali wa utawala wa Assad umeharibika kabisaa kiasi cha kutokarabatika,lakini alionya kuwa bado unaweza kuendelea kun'gan'gania madarakani. Brahimi alisema vikosi vya serikali na waasi wote wanatenda uhalifu katika mgogoro huo.

Baraza la usalama bado limegawanyika

Lakini balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Suzan Rice, alisema masuala ambayo yamekuwa yakiligawa baraza la usalama yameendelea kuwepo na hivyo hakuna njia rahisi ya kusonga mbele.Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limekabiliwa na mkwano juu ya Syria kwa zaidi ya mwaka moja.Urusu na China zimetilia guu maazimio matatu ya Baraza hilo yaliolenga kulaani ukandamizaji unaofanywa na utawala wa rais Assad.

Urusi inazishtumu nchi za magharibi kwa kutaka kubadilisha utawala nchini Syria kwa nguvu,na inasisitiza kuwa haiwezi kumlaazimisha Assad kuachia madaraka. Marekani na washirika wake wanaunga mkono msimamo wa upinzani,kuwa hakuwezi kuwa na mazungumzona Assad.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe,rtre,dape, dpae
Mhariri: SaumYusuf