1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Netanyahu: Vita vitaendelea baada ya usitishwaji mapigano

23 Novemba 2023

Idara ya Usalama wa Taifa nchini Israel imesema mazungumzo ya kusitisha mapigano kati yao na Hamas bado yanaendelea na kueleza kwamba hakutakuwa na mateka atakayeachiliwa kabla ya kesho Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4ZLPp
Mashambulizi ya Israel dhidi ya Hamas
Wapalestina wakiwa wameketi kwenye vifusi vya nyumba iliyoharibiwa kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel kwenye mji wa Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, Jumatano, Novemba 22, 2023.Picha: Mohammed Dahman/AP/picture alliance

Israel Imetoa taarifa hiyo, wakati Rais Joe Biden wa Marekani akiendelea kusisitizia umuhimu wa kuimarisha hali ya utulivu katika eneo la mpaka na Lebanon pamoja na Ukingo wa Magharibi. 

Mshauri wa masuala ya Usalama wa Taifa nchini Israel Tzachi Hanegbi amesema usiku wa jana kwamba mazungumzo ya kusitisha mapigano na Hamas yanaendelea na hakutakuwepo na mateka watakaoachiliwa huru hadi kesho Ijumaa, ingawa hakutoa maelezo zaidi juu ya kusogezwa mbele muda wa kuachiwa mateka hao na haikujulikana mara moja ni lini usitishwaji wa mapigano utaanza kutekelezwa.

Soma pia:Usitishwaji vita kati ya Israel na Hamas wacheleweshwa

Shirika la utangazaji la umma la Israel Kan, limemnukuu afisa mmoja nchini humo kuwa makubaliano hayo yalicheleweshwa kwa saa 24 kwa sababu hayakutiwa saini na Hamas na Qatar, waliosaidia kufanikisha makubaliano hayo na kuongeza kuwa wana imani kwamba makubaliano hayo yatatekelezwa baada ya kusainiwa.

Katika hatua nyingine, Rais wa Marekani Joe Biden amezungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu pamoja na viongozi wa Qatar na Misri, baada ya kuidhinishwa kwa makubaliano hayo ya kuachiliwa mateka mapema jana Jumatano, hii ikiwa ni kulingana na Ikulu ya White House.

Biden amehimiza umuhimu wa kuimarisha kwa utulivu katika eneo la mpaka na Lebanon pamoja na Ukingo wa Magharibi wakati alipozungumza na Netanyahu. Viongozi hao wawili walizungumza baada ya Baraza la Kivita kuidhinisha makubaliano hayo ya siku nne, ambapo Netanyahu alisisitiza kwamba vita hivyo bado vitaendelea baada ya muda wa kusitisha mapigano kumalizika.

Gaza baada ya mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Hamas
Watu wanaonakena wakiwatafuta manusura kufuatia mashambulizi ya Israel kwenye eneo la Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza mnamo Novemba 22, 2023, katikati ya vita vinavyoendelea kati ya Israel na vuguvugu la Hamas la Palestina.Picha: Mohammed Abed/AFP

Netanyahu: Vita vitaendelea hadi kuliangamiza kundi la Hamas

"Nataka kuwa wazi. Vita vinaendelea. Tutaendeleza mpaka tutimize malengo yetu ya kuwarudisha mateka wetu wote, kuwaondoa Hamas na kuhakikisha kwamba baada ya Hamas, Gaza haitadhibitiwa na chama kinachounga mkono ugaidi."

Biden alipozungumza na Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi, amesema Marekani haitaruhusu Wapalestina kulazimishwa kuhama kutoka Gaza ama Ukingo wa Magharibi na hata kuchorwa upya kwa mipaka ya Gaza.

Soma pia:EU: Tufikirie mustakabali katika eneo la Ukanda wa Gaza

Na alipozungumza na Emir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, viongozi hao wawili wamekubaliana kuendelea kuwasiliana ili kuhakikisha makubalino hayo yanatekelezwa klikamilifu. Qatar ina mahusiano thabiti na mataifa hayo yote mawili.

Mbali na makubaliano hayo, kwenye uwanja wa mapambano, ndege za kivita za Israel zimeshambulia miundombinu ya kundi la Hezbollah huko Lebanon usiku wa kuamkia leo, jeshi la taifa hilo limesema.

Jeshi hilo aidha limesema kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba ndege pamoja na vikosi vyake vimeshambulia magaidi waliojaribu kurusha roketi katika eneo la Israel na kuwafyatulia risasi wanajeshi wake. Hezbollah, imesema karibu wapiganaji wake watano waliuawa katika shambulizi hilo, ikiwa ni pamoja na mtoto wa Mohammad Raad, ambaye ni mwenyekiti wa tawi la Hezbollah katika bunge la Lebanon.

Kwa upande mwingine, waasi wa Houthi nchini Yemen wamesema wamerusha makombora ya masafa marefu kuelekea kusini mwa israel, ikiwa ni pamoja na mji wa Bahari ya Shamu wa Eilat. Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran limefanya karibu mashambulizi sita ya angani dhidhi ya jeshi la Israel, IDF tangu kuzuka kwa mapigano kati ya Israel na Hamas, Oktoba 7.