Iran yakanusha kuwasaidia waasi wa Houthi
20 Novemba 2023
Iran imepuzilia mbali madai ya Israel iliyoyaita batili kwamba waasi wa Houthi wanafanya kazi kwa ushirikiano na serikali ya Iran wakati walipoiteka meli inayomilikiwa na ya mfanyabiashara mmoja wa Israel katika bahari ya Shamu.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya nchi za nje wa Iran Nasser Kanani, amesema waasi wa Houthi wanawakilisha mataifa yao na wanachukua hatua kwaajili ya manufaa ya mataifa yao.
Ameongeza kuwa utawala wa Israel hautaki kukubali umepata pigo kubwa katika vita vyake dhidi ya Palestina na unatafuta sababu za kuhalalisha kushindwa kwake kwa kuishutumu Iran.
Soma pia:Ujerumani yapekua nyumba zinazohusishwa na harakati za Iran
Waasi wa Houthi waliiteka meli hiyo ya Galaxy Leader jana Jumapili, siku chache baada ya kutishia kulenga meli za Israel katika bahari hiyo kufuatia vita inavyoviendeleza dhidi ya kundi la wanamgambo la Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Kulingana na taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, meli hiyo ilitekwa na waasi wa Houthi kupitia muongozo uliotolewa na Iran.