1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yaanza siku 3 za maombolezo

4 Julai 2016

Iraq imeanza siku 3 za maombolezo ya kitaifa kwa watu 142 waliouawa katika shambulizi la kujitoa muhanga mjini Baghdad Jumapili asubuhi. Waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi ameapa kuwaadhibu waliolifanya shambulio hilo.

https://p.dw.com/p/1JIXC
Wakazi wa Baghdad katika eneo lililoshambulia.
Wakazi wa Baghdad katika eneo lililoshambulia.Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Mohammed

Siku hizo tatu za maombolezo ya kitaifa zilitangazwa na Waziri Mkuu Haider al-Abadi alipotembelea eneo lililokofanyika shambulio hilo, katika wilaya ya Karrada yenye biashara nyingi. Watu walikuwa wamejazana katika maduka ya eneo hilo, wakinunua bidhaa za matayarisho ya Idd el-Fitr baadaye wiki hii, mashambulizi hayo yalipotokea.

Kiongozi huyo wa Iraq alisema na hapa namnukuu, ''Naelewa hisia za watu, na vitendo vilivyofanywa wakati wa hasira na machungu makubwa''.

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS lilitoa tangazo likidai kuhusika na mashambulizi hayo. IS ilisema katika tangazo hilo kuwa mripuaji alikuwa raia wa Iraq, na kuongeza kuwa alikuwa katika kile kundi hilo lilichokiita ''Operesheni ya kiusalama''. Aidha, IS ilisema ilikuwa ikiwalenga waislamu wa madhehebu ya Shia, ambao inawachukulia kama watu waliopotoka, na imekuwa ikiwaandama kwa mashambulizi yake mjini Baghdad na kwingineko.

Kisasi cha kupokonywa Fallujah?

Shambulizi hilo lilifanyika wiki moja baada ya jeshi la serikali kuukomboa mji wa Fallujah kutoka mikononi mwa IS, ambayo sasa inabakiwa na udhibiti wa mji wa Mosul pekee nchini Iraq.

Kundi la IS limedai kuhusika na shambulio hilo kubwa kuliko yote mwaka huu nchini Iraq.
Kundi la IS limedai kuhusika na shambulio hilo kubwa kuliko yote mwaka huu nchini Iraq.Picha: picture alliance/AP Photo

Mbali na kutangaza siku tatu za maombolezo, Waziri Mkuu al-Abadi pia ameamuru mabadiliko katika mkakati wa usalama mjini Baghdad, mojawapo likiwa kuondoa vifaa vyote bandia vya kugundua mabomu katika vituo vya ukaguzi barabarani.

Wachambuzi wanasema ni kazi ngumu kuzuia mashambulizi haya ya mabomu, ikizingatiwa kuwa maelfu ya magari yanaingia na kutoka mjini Baghdad kila siku.

Lakini pia wananyoshea kidole hitilafu katika sekta ya usalama, ambapo vifaa bandia vya kugundua mabomu vimeendelea kutumiwa katika vituo vya ukaguzi, miaka kadhaa baada ya mfanyabiashara aliyewauzia kukamatwa na kufungwa nchini Uingereza kwa hatia ya kufanya udanganyifu.

Mikakati mipya ya ulinzi na usalama

Waziri Mkuu al-Abadi ameagiza kuharakishwa kwa vituo vyenye mashine za kukagua mabomu kwenye barabara zinazoingia mjini Baghdad, na kupiga marufuku matumizi ya simu za mkononi kwa wafanyakazi kwenye vituo hivyo vya ukaguzi.

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi
Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-AbadiPicha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Mikakati mingine iliyoamuliwa na waziri mkuu al-Abadi ni kupanua matumizi ya ujasusi wa angani, na ushirikiano miongoni mwa taasisi za ulinzi na usalama.

Wiki iliyopita, jeshi la Iraq liliukomboa kikamilifu mji wa Fallujah ulio umbali wa KM 50 Magharibi mwa mji mkuu, Baghdad, ambao ulikuwa umekamatwa na IS mwaka 2014, na kugeuzwa kuwa ngome muhimu ya kundi hilo la kijihadi.

Kwa wakati huu jeshi la Iraq linaelekeza mtutu katika mji wa Mosul, ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini humo, na wa mwisho mkubwa ambao unasalia chini ya udhibiti wa kundi la IS.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/ape

Mhariri: Grace Patricia Kabogo