1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fallujah yakombolewa kutoka kwa IS

19 Juni 2016

Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi amesema vikosi vya Iraq vimeukomboa mji wa Fallujah kutoka kwa wapiganaji wa kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS.

https://p.dw.com/p/1J9Pr
Wanajeshi wa Iraq baada ya kuikomboa Fallujah
Wanajeshi wa Iraq baada ya kuikomboa FallujahPicha: Reuters/T. Al-Sudani

Akitoa tangazo hilo kwa njia ya televisheni, Al-Abadi amesema vikosi hivyo vimelidhibiti eneo la katikati mwa Fallujah hapo jana, yakiwemo majengo ya serikali pamoja na hospitali kuu ya mji huo, ambao ulikuwa ngome muhimu ya mwisho ya IS katika jimbo la Anbar, magharibi mwa Baghdad. Baada ya kuukomboa vikosi vya Iraq viliipandisha bendera ya nchi hiyo katika eneo kuu la serikali ya mji huo.

Hata hivyo, amesema baadhi ya wapiganaji wa IS bado wamebakia katika maeneo ya karibu hasa kaskazini mwa Fallujah. Vikosi vya usalama vimesema kuwa wapiganaji hao wa jihadi wamejiingiza katika misafara ya raia ambao wanayakimbia makaazi yao.

Al-Saadi amesema wanajeshi wa Iraq walikumbana na mapambano ya kawaida katika mashambulizi hayo ya kuukomboa mji huo na hivyo sasa wanaudhibiti mji huo kwa asilimia 80. Imeelezwa kuwa mapigano yalikuwa yanaendelea katika mji wa Fallujah, ambako ndege za kivita za Marekani na Iraq zilikuwa zikiwalenga wapiganaji wa jihadi pamoja na maeneo mengine ya IS.

Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi
Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-AbadiPicha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Watu 50,000 walikwama Fallujah

Mashirika ya kutoa misaada yanakadiria kuwa raia 50,000 walikuwa wamekwama ndani ya mji wa Fallujah wakati mashambulizi yalipoanza wiki kadhaa zilizopita na raia 30,000 hadi 42,000 kati yao wamekimbia tangu wakati huo. Wengi wao wamekuwa wakiishi katika kambi ya karibu na mji huo.

Fallujah ulikuwa mji wa kwanza wa Iraq kuangukia mikononi mwa kundi la Dola la Kiislamu Januari 2014. Vikosi vya Iraq vimekuwa vikisonga mbele kwa msaada wa mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Marekani pamoja na kikosi cha anga cha Iraq. Mashambulizi ya Fallujah yamekuwa yakifanywa na vikosi vya Iraq ambavyo ni vya jeshi, kikanda, shirikisho la polisi pamoja na kikosi maalum cha kupambana na ugaidi.

Wakaazi wa Fallujah wasio na makaazi
Wakaazi wa Fallujah wasio na makaaziPicha: Getty Images/AFP/M. Al-Dulaimi

IS bado inaudhibiti mji wa Mosul ulioko eneo la kaskazini. Al-Abadi amesema operesheni hiyo sasa inaelekezwa katika jitihada za kuukomboa mji wa Mosul, ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Iraq na ngome kuu ya mwisho kwa IS nchini humo.

Kamanda mkuu wa operesheni hiyo, Luteni Jenerali Abdulwahab al-Saadi, amesema vikosi maalum vilikuwa vinaendeleza harakati zao za kuwaondoa kabisa wapiganaji wa IS kutoka kwenye mji huo.

Iraq imetangaza kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wataungana na vikosi vya Kikurdi kuanza kuuzingira mji wa Mosul kuanzia eneo la kusini. Operesheni hiyo pia itasaidiwa kwa mashambulizi ya anga yatakayoongozwa na Marekani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,AP
Mhariri: Isaac Gamba