Iran yataka vikosi vya kigeni viondoke Ghuba
22 Septemba 2019Haya yanakuja wakati ambapo mkataba wa nyuklia wa nchi hiyo na nchi zenye nguvu duniani unasambaratika na Marekani imetuma vikosi zaidi kwa ajili ya kuongeza usalama kwa washirika wake wa Kiarabu.
Akizungumza wakati wa gwaride la kijeshi, Rais Hassan Rouhani amesema kwamba uwepo wa majeshi ya kigeni katika Ghuba huenda ukasababisha matatizo kwa usalama wa nishati duniani.
Amesema Iran inaunyoosha "mkono wa urafiki na udugu" kwa mataifa mengine ya kanda hiyo kwa kusimamia usalama katika Ghuba ya Uajemi na njia ya bahari ya Hormuz ambapo asilimia ishirini ya mafuta yanayouzwa nchi za nje yanapitia.
Iran imekanusha kuhusika na kuishambulia Saudi Arabia
Marekani imesema kwamba Iran ndiyo iliyohusika na msururu wa mashambulizi katika miundombinu muhimu ya mafuta katika kanda hiyo, ikiwemo mashambulizi yaliyofanywa kwa ndege zisizokuwa na rubani katika miundombinu ya uzalishaji mafuta huko Saudi Arabia, mashambulizi yaliyotikisa masoko ya nishati duniani.
Iran imekanusha madai hayo na kusema mashambulizi yoyote ya kulipiza kisasi yatakayofanywa na Marekani yatasababisha kuanza kwa vita.
Kufuatia mashambulizi hayo, rais Donald Trump wa Marekani alikuwa amezungumzia uwezekano wa kujibu kijeshi ambapo aliandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba Marekani iko tayari kabisa.
Baadae, Marekani ilitangaza nyongeza ya vikwazo kwa Iran kwa kuilenga benku kuu ya nchi hiyo.
Siku ya Ijumaa Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mark Esper alitangaza kuwa Marekani inatuma nguvu mpya ya majeshi kwa Saudi Arabia baada ya ombi la nchi hiyo ya kifalme, akisema kuwa vikosi hivyo vya jeshi vitashughulika na masuala ya ulinzi na hasa ulinzi dhidi ya makombora ya angani.
Rais Rouhani anatarajiwa kusafiri kwenda Ney York Jumatatu
Pamoja na kuongeza idadi ya wanajeshi na vifaa vya kijeshi kwa Saudi Arabia na nchi za Umoja wa Kiarabu, Marekani inaongoza muungano wa kijeshi wa majini ambao unaojumuisha nchi za Umoja wa Kiarabu, Saudi Arabia, Bahrain, Uingereza na Australia ili kuimarisha usalama wa njia za majini za eneo hilo na njia zengine muhimu za biashara ya mafuta.
Kwa muda mrefu Iran imetaka kuondolewa kwa vikosi vya majeshi ya nchi za Magharibi na Marekani kutoka nchi za Kiarabu zilizo katika eneo la Ghuba kwa kuwa inaona hatua hiyo kama kitisho kinachoikodolea macho nchi hiyo.
Rais Hassan Rouhani anatarajiwa kusafiri kuelekea mjini New York hapo Jumatatu, siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Rouhani amesema kuwa atatoa mpango wa amani wa kanda hiyo katika Baraza hilo la Umoja wa Mataifa wakati ambapo wasiwasi unaongezeka kati ya Iran na Marekani kufuatia kusambaratika kwa mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Javad Zarif ambaye amewekewa vikwazo na Marekani, tayari amewasili New York kuelekea mkusanyiko huo wa viongozi wa dunia unaofanyika kila mwaka.