Iran yasema vikwazo vya Marekani 'havikubaliki'
16 Mei 2019Mvutano tayari ulikuwa mkubwa baada ya Rais Donald Trump kujiondoa katika mkataba wa nyuklia mwaka mmoja uliopita. Lakini umeongezeka hata zaidi katika wiki za karibuni baada ya Marekani kupeleka kikundi cha manowari zake za kivita katika Ghuba ya Uajemi kuhusiana na ilichodai kuwa ni vitisho vya Iran.
Akizungumza leo mjini Tokyo ambako anafanya mazungumzo na maafisa wa Japan, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema kuwa hatua ya Marekani kuongeza mvutano huo haikubaliki.
Matamshi ya Zarif yamekuja saa chache tu baada ya Marekani kuaamuru wafanyakazi wake wasiokuwa na majukumu ya dharura kuondoka katika ubalozi wake wa Baghdad, Iraq kutokana na kile ilichokitaja kuwa ni kitisho kutoka kwa wanamgambo wa Iraq wanaoungwa mkono na Iran.
Hatua hiyo imeongeza hofu kuwa mahasimu hao wa muda mrefu huenda wakaanzisha vita licha ya pande zote mbili kusisitiza kuwa hazina nia ya vita.
Trump, hata hivyo, amebashiri kuwa Iran hivi karibuni itataka kufanya mazungumzo na akakanusha kuwa kuna hali ya kutolewana katika Ikulu ya Marekani kuhusu hatua ambazo wakosoaji wanasema huenda zikasababisha vita katika Mashariki ya Kati.
Wapinzani wa Trump wanasema kuwa watu wenye misimamo mikali wakiongozwa na mshauri wa usalama wa taifa John Bolton, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiunga mkono kuangushwa kwa utawala wa Iran, wanashinikiza nchi hiyo kuingia vitani.
Marekani inasema kuwa imepata taarifa za kijasusi kuhusu uwezekano wa mashambulizi kufanywa na Iran au wanajeshi wanaoungwa mkono na Iran, yakivilenga vituo vya Marekani nchini Iraq au Syria.
Lakini tangu kutolewa onyo la kwanza la Marekani mnamo Mei 5, tukio pekee limekuwa ni shambulizi la kutatanisha la Jumatatu wiki hii kwenye meli za mizigo katika bandari ya Fujairah, ya Umoja wa Falme za Kiarabu.
Wakati huo huo, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umefanya leo mashambulizi katika ngome ya waasi wa Huthi nchini Yemen. Mashambulizi hayo yamekuja baada ya waasi hao wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran kudai kuhusika na mashambuluzi ya ndege zisizoruka na rubani siku ya Jumanne ambayo yaliharibu bomba la mafuta la Saudia.