1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran, Uturuki zalaani makubaliano ya Israel na UAE

14 Agosti 2020

Uturuki na Iran zimeukosoa Umoja wa Falme za Kiarabu UAE kutokana na hatua yake ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Israel. Uturuki imeitaja hatua hiyo kuwa usaliti na Iran ikisema ni upumbavu wa kimkakati.

https://p.dw.com/p/3gzPl
Palästina | Annäherung zwischen Israel und den Vereinigten Arabischen Emiraten | Protest in Nablus
Picha: Reuters/R. Sawafta

Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imesema historia na dhamira ya watu wa kanda ya Mashariki ya Kati havitasahau na wala kusamehe kile ilichokiita kitendo cha unafiki kilichofanywa na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Taarifa hiyo imeongeza kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu umefanya hivyo kwa maslahi yake finyu ili kuunga mkono mpango batili wa Marekani.

Soma pia Ujerumani yaonya dhidi ya unyakuzi wa Israel.

Kwa upande wake,  wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema upumbavu huo wa kimkakati utaimarisha tu upinzani dhidi ya Israel. Serikali mjini Abui Dhabi iliwadanganya watu wa Palestina kwa uamuzi huu wa aibu, haramu na wa hatari wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel,"  imeendelea kusema taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Iran, na kuongeza kuwa Wapalestina hawasamehi makubaliano hayo na utawala wa kihalifu wa Israel.

Palästinenser Verbrennung Bilder von Abu Dhabi Kronprinz und israelische Ministerpräsident Netanjahu
Wapalestina wakichoma picha za waziri mkuu wa Israel na mrithi wa kiti cha ufalme wa Abu Dhabi Mohammed bin Zayed al-Nahyan, wakati wa maandamano ya kupinga makubliano kati ya Israel na UAE.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Mohammed

Makubaliano hayo, ambayo yaliratibiwa na utawala wa rais wa Marekani Donald Trump, yanaufanya Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa taifa la kwanza la Kiarabu katika kipindi cha karibu miaka 26, kulitambua taifa la Kiyahudi la Israel.

Wapalestina wamelaani tangazo la makubaliano hayo na kumuita nyumbani balozi wao wa Umoja wa Falme za Kiarabu. Kufuatia makubaliano hayo, Israel imesitisha mpango wake wa kusogeza mamlaka yake katika maeneo inayoyakalia katika Ukingo wa Magharibi.

Soma pia Israel na UAE kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia

Serikali ya Uturuki mjini Ankara imeikosoa zaidi UAE kwa kudhoofisha mazungumzo ya amani katika kanda ya Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa taifa hilo halina mamlaka ya kujadili na Israel katika jina la Wapalestina.

"Kwa hakika, kushindwa kwa wale waliowasiliti watu wa Palestina na harakati zao watabaki katik vitabu vya historia," msemaji wa rais Recep Tayyip Erdogan Ibrahim Kalin aliandika katika ukura wa Twitter.

Baadhi ya mataifa yapongeza makubaliano na kusema huenda yakaleta utulivu Mashariki ya Kati

Russland: Außenminister Maas in Moskau
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko MaasPicha: picture-alliance/AP/Russian Foreign Ministry Press Service

Uhusiano wa Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu uliingia doa baada ya shambulizi na waandamanaji wa Kiiran dhidi ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Tehran mwaka 2016. Mwitikio kutoka barani Ulaya hata hivyo ulikuwa chanya, ambapo msemaji wa halmashauri kuu ya umoja wa Ulaya Nabila Massrali amesema "kurejesha uhusiano kutanufaisha pande zote, na ni muhimu kwa pande zote, na pia kwa utulivu wa kikanda.

Soma pia Misri, Ufaransa, Ujerumani na Jordan zaionya Israel

Waziri wa mambo ya nje wa ujerumani Heiko Maas amesema amempongeza mwezake wa israel kwa hatua hii ya kihistoria.

Ufaransa pia imekaribisha makubaliano hayo, ikiseka mataifa yote mawili yalikuwa washirika muhimu katika kanda hiyo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufransa Jean-Yves Le Drian, amesema mpango wa Israel wa kuyatwaa maeneo ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi uliositishwa kama sehemu ya makubaliano hayo, unapaswa kufutwa milele.

Sweden pia imekaribisha makubaliano kama hatua chanya kwa ajili ya mazungumzo kati ya Waisrael na wapalestina.

Chanzo: dpa,ap