Inamaanisha nini kuwa polisi wa kike Nigeria?
16 Machi 2011Ufisadi na ukandamizaji ndio picha waliyonayo Wanigeria wengi kuhusu polisi. Kazi hii ilikuwa inakumbana na unyanyapaa.
"Ndivyo ilivyokuwa mtu anapofikiria kazi ya upolisi. Nilipoanza kazi mwaka 1984, mtu akichukuwa kazi hii anatazamwa kwa mshangao, kwa nini afanye kazi hii, na mshangao zaidi unakuja pale mwanamke anapochagua kazi hii. Lakini taratibu wakati unabadilika. Sasa kila mtu anataka kuwa polisi, maana kumeanza kuwa na hisia nzuri kuhusu upolisi." Ndivyo anavyosema Waziri wa Polisi wa Jimbo la Jigawa la Kaskazini mwa Nigeria, Hashin Gungu.
Hivi sasa kuna askari polisi wa kike 221 wanaofanya kazi chini ya Gugu, ikiwa ni asilimia 50 zaidi ya hapo nyuma. Lakini bado kuna changamoto zake.
Wengi wanaamini kuwa askari mwanamke hawezi kuolewa. Inapotokezea kuolewa, basi huyo mwanamme anapaswa kufanyiwa uchunguzi rasmi na serikali, kuangalia, kwa mfano, tabia zake, wasifu wake na rekodi yake.
Kwa kufanya hivi, serikali inakusudia kuona kwamba idara ya polisi haitumiliwi na wahalifu kupitia njia za panya, na kwa Salomi Bako, ambaye ni askari polisi wa kike, hilo si tatizo.
Anasema madhali tu mtu amefuata masharti na maelekezo yote, apati shida yoyote, kama alivyofuata yeye alipotaka kuolewa.
Kwa kiwango kikubwa, askari wanaume na wanawake wanafanya kazi sawa, ingawa zipo baadhi ya kazi ambazo wanazifanya wanaume tu.
Na inapotokezea kazi hizo zikafanywa na mwanamke, kama vile zamu za usiku na kuhudumu mwisho wa wiki, basi huhisabiwa kwenye mshahara wake. Jambo hilo linawaridhisha askari polisi wengi wa kike.
"Kwangu kazi ya polisi inanipa faraja sana, kwa sababu sasa wamebadiisha masharti. Na hilo mtu analiona kwenye mishahara. Sasa ni mkubwa zaidi kuliko mwanzoni. Unaleta tafauti katika maisha yako. Nasi tumefaidika vizuri na mabadiliko haya." Anasema Koplo Naomi Williams.
Lakini pia, kuna kazi nyengine ambazo hufanywa na askari mwanamke tu, kama vile kuwasachi washukiwa wa kike au kukabiliana na maandamano na migomo ya wanawake au watoto.
Imam Kassim Ramadhan wa Kano anasema kwenye Uislamu, mwanamke ana haki kamili za kiraia, ikiwemo hii ya kufanya kazi aitakayo.
"Uislamu hausemi kamwe kwamba wanawake wanazuiwa kufanya kazi ya upolisi au afisa wa usalama, bali ni wajibu hasa. Ikiwa watu wenyewe hawafanyi kazi hizi, watakuja wengine wazifanye na waingilie mambo yetu. Mtu anapokuja kupekua nyumbani mwako, na yeye si Muislamu, anaweza asiheshimu utamaduni wako.
"Lazima uwe na mtu ambaye anaujua utamaduni wako, anazungumza lugha yako na ana uhusiano na wewe. Huyo unaweza kufanya kazi naye kirahisi. Kwa hivyo, sioni sababu kwa nini wanawake wasifanye kazi ya upolisi. Sisi tunalipokea vyema jambo hili." Anasema Imam Kassim.
Katika majimbo yenye Wakristo wengi ya Kusini, kuna mwamko mkubwa zaidi wa ushiriki wa wanawake kwenye jeshi la polisi. Waziri wa Polisi wa Jimbo la River, Suleiman Abba, anasema kuwa huko hakuna suala la ujinsia katika jeshi la polisi.
Bali kuna kinyume chake hasa, maana robo nzima ya polisi wa jimbo hilo ni wanawake, na wanapewa kazi zile zile wanazofanya wanaume.
Mwandishi: Gwendolin Hilse/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman