Zaidi ya watu 200 wauawa Nigeria
2 Februari 2011Katika ripoti yake, shirika hilo la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, limesema machafuko hayo ya hivi karibuni yaliyosababisha mauaji yalichochewa na mfululizo wa mabomu katika mkesha wa sikukuu ya Krismasi katika jamii mbili huko Jos, mji mkuu wa jimbo la Plateau. Tangu wakati huo Waislamu na Wakristo kadhaa wameuawa katika mazingira ya kutisha na sababu hasa ikiwa ni udini pamoja na ukabila.
Kwa mujibu wa shirika hilo la kimataifa, miongoni mwa watu waliouawa ni watoto, ambao wengi wao wameuawa kwa kuchomwa moto. Mauaji hayo ya hivi karibuni yanafuatia machafuko yaliyofanyika mwaka 2010 na kusababisha mauaji ya watu 1,000 katika jimbo hilo.
Human Rights Watch imesema kuwa serikali ya Nigeria lazima ichukue hatua sahihi za kuwalinda raia wake wa makabila yote na mashambulio zaidi au mauaji na kumruhusu mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulika na masuala ya kuzuia mauaji ya halaiki, Francis Deng, kulitembelea jimbo la Plateau, kwa lengo la kusaidia kuleta amani katika jimbo hilo.
Septemba mwaka uliopita, Deng aliomba rasmi kupatiwa idhini na serikali ya Nigeria ili kuitembelea Jos mwezi Oktoba lengo likiwa kuwasaidia viongozi wa kijamii kuchukua hatua za kupunguza hatari ya kuongezeka kwa ghasia. Hata hivyo, serikali ya Nigeria haijajibu rasmi ombi hilo wala kumruhusu mjumbe huyo kufanya kazi yake hiyo.
Kwa mujibu wa viongozi wa kijamii mjini Jos, mashambulio ya mkesha wa Krismasi katika makanisa mawili mjini Jos na siku kadhaa za machafuko ya kidini yaliyofuatia mashambulio hayo ya mabomu, yalisababisha mauaji ya watu 107. Mtandao wa wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu umechapisha taarifa iliyotolewa na kundi la wapiganaji la Boko Haram lenye makaazi yake kaskazini mwa Nigeria likidai kuhusika na mashambulio hayo.
Mauaji hayo ya kulipiziana kisasi yaliendelea hadi Janauri mwaka huu wa 2011. Vijana wanane wa Kiislamu waliokuwa katika gari wakielekea kwenye harusi, walishambuliwa Januari 7 baada ya kupita njia tofauti na kujikuta wakiishia katika kijiji cha Wakristo cha Barkin Ladi. Siku iliyofuata ya Januari 8, vijana wa Kiislamu mjini Jos waliwashambulia ovyo Wakristo, wengi wao wakiwa wafanyabiashara wa kabila la Igbo katika soko la Dilimi na katika barabara ya Bauchi.
Mtafiti wa ngazi ya juu wa Human Rights Watch katika eneo la Afrika Magharibi, Corinne Dufka, anasema kuwa Serikali ya shirikisho na Jimbo la Plateau lazima zichukue hatua madhubuti kumaliza ghasia hizo kwa kuondoa sera za kibaguzi katika ngazi ya majimbo na serikali za mitaa, ambazo ndio zinachochea mivutano. Aidha, Dufka ametaka uchunguzi wa kina ufanyike na kuwafungulia mashtaka wahusika wote wa ghasia hizo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (HRW)
Mhariri: Miraji Othman