Huyu ndie Li Keqiang Mwanadiplomasia wa China
27 Oktoba 2023
Waziri mkuu wa zamani wa China Li Keqiang amefariki dunia baada ya kupata shambulizi la moyo mapema hii leo.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la nchini humo Li Keqiang amekutwa na umauti baada ya kupatwa ghafla na shambulio la moyo.
Kulingana na taaarifa hiyo, waziri mkuu huyo wa zamani alianza kuugua Alhamisi na alikufa baada ya juhudi za kuokoa maisha yake kushindikina.
Soma zaidi:Waziri Mkuu wa zamani wa China Li Keqiang amefariki dunia
Li Keqiang aliyekuwa na umri wa miaka 68 amefariki dunia ikiwa ni miezi 10 tangu kustaafu kwake katika shughuli za kiserikali.
Alikuwa waziri mkuu na kiongozi wa baraza la mawaziri chini ya rais Xi Jinping kwa miaka kumi hadi alipojiuzulu mwezi Machi.
Afya yake ilidhoofika kwa muda mrefu
Kwa miaka mingi kumekuwa na uvumi kuhusu afya ya kiongozi huyo. Baadhi ya wanadiplomasia waliwahi kusema katika mazungumzo ya faragha kuwa, wakati wa ziara zake nje ya China ratiba za LiKeqiang zilitawaliwa na vipindi virefu vya mapumziko.
Wizara ya mambo ya nje ya China, kupitia msemaji wake Mao Ning imesema inaomboleza kifo cha kiongozi huyo.
´´Mipango na mikakati ya kuupumzisha mwili wa kiongozi wetu itatolewa baadae, tutatangaza kama kutakuwepo kwa wanasiasa wakuu wa kigeni wanaokuja na kuhusu mipango ya mazishi, tutaitangaza kwa wakati usio mrefu´´ alisema msemaji huyo.
Msemaji huyo ameongeza kwamba katika kipindi cha miaka 10 akiwa kama Waziri Mkuu chini ya Xi, Li alifanya majukumu yake katika kiwango cha juu na cha kisasa zaidi hasa katika kuunga mkono mageuzi ya kiuchumi.
Mnamo mwaka 1966 hadi 1976, Li akiwa kijana alikuwa akifanya kazi kama kibarua katika mashamba katika mkoa maskini wa Anhui mashariki mwa China, baadaye alipata shahada ya sheria katika chuo kikuu cha Peking ambapo wanafunzi wenzake wanasema Li alipenda sana nadharia ya kisiasa ya kiliberali ya nchi za magharibi.
Soma zaidi: Merkel aitaka China kuzungumzia haki za binaadamu
Katikati ya miaka ya 1980, Li alianza kupata umaarufu uliopelekea kuchaguliwa kuwa msimamizi mkuu wa wanafunzi wenzake , Baadaye Li alipanda ngazi hadi kuwa afisa mkuu wa Chama tawala cha Kikomunisti katika jimbo la Henan, na Liaoning, kaskazini-mashariki mwa China na maeneo hayo yaalishuhudia ukuaji mkubwa wa uchumi chini yake.
Li Mwanasheria aliyeimarisha uchumi wa China
Pamoja na hatua hizo muhimu lakini sifa zake ziliharibiwa na jinsi alivyoshughulikia janga la virusi vya UKIMWI lililotokana na mpango mbovu wa uchangiaji damu alipokuwa mkuu wa chama katika jimbo la Henan.
Mwaka 2013, Li alieuliwa kuwa Waziri Mkuu , majaribio yake ya kukabiliana na changamoto kubwa za kiuchumi za China yalipunguza mamlaka makubwa ya Xi, ambaye awali alionekana kama mpinzani wa uongozi wa nchi hiyo.
Soma zaidi: Xi wa China apongeza 'ushirikiano mpya wa kimkakati' na Colombia
Katika nafasi yake ya Uwaziri Mkuu, Li alisifiwa kwa kusaidia kuivusha nchi katika msukosuko wa kifedha duniani bila kuathiriwa, wakati wake madarakani ulishuhudia mabadiliko ya mamlaka katika uongozi wa rais Xi Jinping.
Mwanafunzi mwenza wa zamani katika Chuo Kikuu cha Peking Guoguang Wu, ambaye sasa ni mtafiti mkuu huko Stanford ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Li "alikuwa mtu mwenye uwezo wa mawazo huru" wakati walipokuwa pamoja.
Lakini akaongeza na kusema
"Alipoingia kuwa afisa wa serikali, uwezo huu wa mawazo huru ulionekana kutoweka. Siamini kuwa ameacha urithi wa kisiasa. Historia itamsahau hivi karibuni."
Wakati Li alipoondoka madarakani,China ilikuwa inakabiliwa msukosuko wa kiuchumi baada ya janga la Uviko 19, Uteuzi wa Li Qiang kama mrithi wake mwaka huu ilionekana kama ishara kwamba ajenda yake ya mageuzi ya kiuchumi ilikuwa imeanguka pua.
Hata hivyo, katika hotuba yake ya mwisho kama Waziri Mkuu Li alisema nadharia yake ya uchumi ilikuwa inafanya vizuri na kwamba lilikuwa ni suala muda tu kuonyesha uwezo mkubwa na kasi ya ukuaji zaidi.