1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua ya Zelenskiy kwa mkuu wa jeshi yazusha wahaka Ukraine

5 Februari 2024

Mashambulizi ya mabomu ya Urusi katika mji wa Kherson kusini mwa Ukraine yamesababisha vifo vya watu 4 Jumatatu na mtu mmoja amejeruhiwa.

https://p.dw.com/p/4c43i
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy aadhimisha siku ya uzalendo wa Ukraine
Volodymyr Zelenskiy (kushoto) na Valerii Zaluzhny (kulia)Picha: Ukrainian Presidential Press Off/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Haya yanafanyika wakati ambapo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy anatafakari kumuachisha kazi mkuu wa jeshi la nchi hiyo kama sehemu ya mabadiliko mapana ya uongozi katika jeshi la nchi hiyo.

Uwezekano huo wa Zelenskiy kumfuta kazi mkuu wa jeshi umelishtua taifa hilo pamoja na marafiki wa Magharibi wa Ukraine ambayo kwa sasa inapambana ili kuishinda Urusi iliyoivamia.

Zelenskiy alithibitisha taarifa hiyo katika mahojianona kituo cha televisheni cha Italia RAI TV yaliyorushwa Jumapili jioni akisema, anatafakari kumuachisha kazi Jenerali Valerii Zaluzhny, amiri jeshi mkuu wa majeshi ya Ukraine ambaye ana umaarufu sana nchini humo.

Waukraine wengi hawajafurahishwa na hatua ya Zelenskiy

Rais huyo amesema anataka kuchukua hatua hiyo kwasababu anataka kuhakikisha kwamba nchi hiyo inaongozwa na watu ambao "wana uhakika wa kuleta ushindi" dhidi ya Urusi.

USA New York | 78. Hadhira Kuu ya UN | Volodymyr Zelenskiy, Rais Ukraine
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskiyPicha: Mike Segar/REUTERS

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani ya Ukraine na mataifa ya Magharibi, Zelenskiy, alimtaka Zaluzhny ajiuzulu wiki iliyopita ila akakataa. Zaluzhny mwenyewe lakini hajatoa tamko lolote hadharani kuhusiana na ripoti hizo.

Ripoti hizo zimezusha malalamiko mengi Ukraine na kuifurahisha Urusi wakati ambapo vita hivyo vinaelekea kuingia mwaka wake wa pili. Zaluzhny anaheshimiwa pakubwa miongoni mwa majeshi ya Ukraine na anachukuliwa kama shujaa wa kitaifa. Anasifiwa kwa kuzuia uvamizi kamili wa Urusi katika siku za mwanzo za vita hivyo na alitumia utaalam wake kuhakikisha kwamba majeshi ya Urusi yanarudishwa nyuma.

Meya wa mji wa Kyiv ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Zelenskiy, Vitalii Klitschko, ameikosoa hatua ya kumuachisha kazi mkuu huyo wa jeshi, akidai kwamba hilo likifanyika basi siasa zitakuwa zimepewa kipau mbele badala ya nia ya nchi.

Haijabainika hasa ni nani atakayeichukua nafasi ya Zaluzhnyna iwapo atapewa heshima ile ile miongoni mwa vikosi vya Ukraine. Kuachishwa kazi kwake huenda kukawashusha mabega majeshi wakati muhimu mno wa vita.

Rasimu ya sheria yakwama bungeni

Kwengineko baadhi ya wanajeshi mashariki mwa Ukraine wanasema hawana budi sasa ila kupigana hadi mwisho wa vita, licha ya juhudi za serikali mjini Kyiv kufanya uhamasishaji wa majeshi zaidi kuchukua nafasi ya wale waliohudumu kwa muda mrefu katika uwanja wa mapambano.

Urusi yalaumiwa kwa kifo cha mkuu wa Wagner

Rasimu ya sheria inayolenga kuongeza idadi na nguvu katika jeshi la Ukraine linalopungua na linalokabiliwa na uchovu, imekwama bungeni ila mojawapo ya mabadiliko yanayopendekezwa ni kuhakikisha kwamba wanajeshi waliopigana kwa miaka mitatu wanapewa nafasi ya kuondoka na kwenda kupumzika.

Rais Zelenskiy amesema jeshi lilipendekeza kuhamasishwa kwa Waukraine kati ya 450,000 hadi 500,000 kujiunga na jeshi hilo kwa ajili ya vita vinavyoendelea. Familia za baadhi ya wanajeshi waliopigana kwa muda mrefu wamemuomba Zelenskiy kuwapa mapumziko, ila wanajeshi karibu na mji ulioharibiwa wa Bakhmut wanaamini hilo haliwezekani.

Vyanzo: APE/AFPE/Reuters