Hatma ya Uingereza yaamuliwa Scotland
18 Septemba 2014Katika siku ya mwisho ya kampeni hapo jana, viongozi kutoka pande zote waliwasihi Wascot kutumia fursa hii ya kihistoria katika kura iliyozigawa familia, marafiki na wapenzi, lakini pia ikalisisimua taifa hilo la wakaazi milioni 5.3. Kuanzia visiwa vya Scotland vya Atlantic hadi kwenye mashamba ya mji wa Glasgow, wapigakura wanaombwa kujibu "Ndiyo" au "Hapana" kwa swali la iwapo Scotland iwe taifa huru.
Waziri mkuu wa Uingereza Davidi Cameron, aliwasihi Wascot kupiga kura ya kubakia katika muungano, na kuonya kuwa kuvunjika kwa muungano huo kutakuwa "talaka yenye maumivu makali" iliyojaa mashaka ya kiuchumi. Ikiwa Wascot watasema ndiyo, huo utakuwa mwisho wa muungano uliyoanza mwaka 1707, na hii inaweza kumlazimu Cameron kujiuzulu, na inaweza kuzuwa maswali mazito juu ya hadhi ya Uingereza katika jukwaa la kimataifa.
Cameron akiri hana ushawishi kwa Scotland
Kibarua cha Cameron kinaweza kuota mbawa ikiwa Scotland itajitenga, lakini waziri mkuu huyo mwenye umri wa miaka 47 amekiri kuwa historia yake ya Kingereza na siasa za kihafidhina vinamaanisha hayuko katika nafasi bora ya kuwashawishi Wascot.
Hilo limeacha uongozi wa hoja ya wanaotetea muungano mikononi mwa chama cha upinzani cha Labour, kilichoshinda viti 41 vya Scotland katika uchaguzi wa mwaka 2010, na chama pekee kilicho na uungwaji mkono ndani ya Scotland, kuwa na uwezo wa kukabiliana na chama NSP kinachoongoza kampeni ya uhuru.
Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Gordon Brown, Mscot ambaye katika wiki za karibuni ameongoza mapambano ya kuubakiza muungano, aliwaonya Wascot mjini Glasgow kwamba kiongozi wa kampeni ya ndiyo Alex Salmond alikuwa anawaingiza kwenye mtego.
"Kuweni na imani, jitokezeni mhesabiwe kesho," brown aliunguruma, huku huku akirusha mikono hewani na kushangiliwa na wanaopenda muungano. "Wambieni marafiki zenu kwamba, kutokana na sababu za mshikamano, ushirikiano, haki na fahari nchini Scotland, jibu pekee ni kupiga kura ya 'Hapana'."
Vigogo wahaha
Wakikabilia na kitisho kikubwa zaidi cha ndani kwa muungano wa Uingereza tangu Ireland ilipojitenga karibu karne moja iliyopita, viongozi wa nchi hiyo, kuanzia waziri mkuu David Cameron hadi vigogo wa biashara na mastaa wa muziki, wameungana katika juhudi za mwisho kuwashawishi Wascot kwamba Uingereza inakuwa bora ikiwa imeungana.
Ikiwa Scotland itaamua kuwa nchi huru leo, itakuwa na muda wa miezi 18 ya mazungumzo na Uingereza juu ya kugawana mafuta yanayochimbwa katika bahari ya Kaskazini, na kujadili uanachama wa Umoja wa Ulaya, na kituo kikuu cha nyambizi za nyuklia za Uingereza kilichoko Scotland.
Scotland inasema itatumia sarafu ya pauni baada ya kupata uhuru lakini London imeondoa uwezekano wa kuwa na muungano rasmi wa sarafu, wakati Uingereza itabidi kuamua nini cha kufanya kuhusu kituo cha nyambizi za nyuklia kilichoko Scotland, ambacho wanzalendo wanataka kukiondoa.
Hofu ya kuvunjika kwa Uingereza, ambayo ndiyo taifa la sita kwa uchumi mkubwa duniani, na mwanachama mwenye kura ya turufu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, imewafanya raia na washirika pia kutafakari juu ya nini kitabakia, huku wafadhili wa mji wa London wakionya juu ya kuvurugika kwa masoko ya fedha.
Kampeni za vitisho
Alex Salmond, kiongozi shupavu wa kampeni ya ndiyo, ameutuhumu utawala mjini London kwa kupanga kampeni ya viongozi wa biashara inayolenga kuwatishia Wascot, baada ya bishara kuanzia kampuni ya mafuta ya BP hadi Standard Life kuonya juu ya hatari za uhuru.
Marekani ilibainisha wazi kuwa inataka Uingereza ibakie kuwa mshirika imara na alieungana, katika maneno ya rais Barack Obama, huku akisema hilo ni chaguo la Scotland. " Natumai watu wa Scotland watachagua kubaki na Uingereza," alisema rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, akionya juu ya hatari zakifedha na mazungumzo ya muda mrefu baada ya kutengana.
Nchini England, Cameron alikiri kwa gazeti la Times kwamba aliamka usiku akitokwa na jasho juu ya uwezekano wa kushindwa nchini Scotland. "Tumepanga namna Scotland inavyoweza kupata kilicho bora katika mazingira yote," Cameron aliwambia waandishi wa habari baadae.
Muundo wa serikali laazima ubadilike
Katika jitihada za kukata makali ya hoja ya Salmond ya kujitenga, viongozi wa Uingereza wameahidi kuihakikishia Scotland viwango vya juu wa ufadhili wa serikali na kuwapa Wascot udhibiti zaidi wa fedha zao.
Viongozi wa Uingereza wanakiri kuwa hata kama Scotland itapiga kura kubakia katika muungano, muungano wa falme hiyo utapaswa kubadilika, kwa sababu kutoa mamlaka kutachochea miito ya kupunguza mamlaka ya serikali kutoka kwa wapigakura nchini England, Wales na Irelanda ya Kaskazini.
Kura ya ndiyo kwa mjukuu
Kuanzia kwenye madirisha ya nyumba za watu hadi kwenye kona za mitaa na hata kwenye vikombe, uungwaji mkono wa kampeni ya 'Ndiyo' umekuwa ukionekana zaidi kuliko ya 'Hapana' katika maeneo mengi ya Scotland.
Wafuasi wa kampeni ya 'Ndiyo' waliokusanyika katika uwanja mkuu wa mjini Glasgow siku ya Jumatano, Frank Evans mwenye umri wa miaka 62 alisema: Nimetawaliwa na serikali za Westminster kwa muda mrefu sana. Hii ndiyo fursa ya kujitawala wenyewe, kwa ajili ya binti yangu na mjukuu wangu."
Mjadala katika kampeni hiyo umejikita zaidi juu ya uchumi. Masuali juu ya iwapo Scotland itakuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, na kwa muda gani hili litachukuwa pia yamejitokeza.
Bunge la Scotland lililofunguliwa mwaka 1999, linahodhi baadhi ya mamlaka yaliyogatuliwa kutoka Westminster, kutunga sera katika maeneo ya ndani kama vile afya na elimu. Hata kama kutakuwa na kura ya 'Hapana', Scotland itapewa mamlaka mapya, yumkini katika maeneo ya kodi na ustawi, ambayo Gordon Browm anasema yatakuwa sawa na kujitawala wenyewe.
Bila kujali matokeo ya kura hiyo, wadadisi wengi wamesifu kiwango cha juu cha ushiriki wa kisiasa kilichonesha katika kampeni. "Ni tukio lililoamsha hamasa nchini Scotland kuliko kitu kingine katika siasa," alisema Magnus Gardham, mhariri wa siasa wa gazeti la Scotland la "The Herald."
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe.
Mhariri: Sekione Kitojo