1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya uhuru wa Scotland itaiathiri michezo?

15 Septemba 2014

Wakati kura ya maoni kuhusu uhuru wa Scotland ikikaribia kupigwa, kuna mambo mengi yanayozingatiwa katika mdahalo kati ya wale wanaopiga kura ya kuunga mkono uhuru, na wanaotaka Scotland ibakie sehemu ya Uingereza.

https://p.dw.com/p/1DCWI
Trikots Olympia Großbritannien
Picha: picture-alliance/Photoshot

Sekta ya michezo pia ni miongoni mwa yanayojadiliwa. Kwa mfano,wanariadha wa Scotland kwa sasa huiwakilisha Uingereza – Team GB – katika michezo ya Olimpiki. Wanariadha 55 wa Scotland walikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya Uingereza iliyoshiriki Michezo ya Olimpiki jijini London mwaka wa 2012 ikiwa ni karibu asilimia 10 ya jumla ya wawakilishi.

Hivyo basi ni nini kinachoweza kufanyika katika michezo ya siku za usoni ya Olimpiki kama Wascotland watapiga kura ya kujipa uhuru?

Kura hiyo inaweza kuthibitishwa rasmi mnamo Macho 2016. Na hiyo itamaanisha kuwa kutakuwa na miezi michache iliyosalia kabla ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Rio mnamo Agosti 5, hali itakayokuwa na athari kubwa kwa timu ya Scotland kuwatuma wanariadha wake kwa wakati unaofaa.

Schottland Unabhängigkeit Marsch des Oranierordens in Edinburgh 13.09.2014
Maandamano ya kuunga mkono kura ya wanaotaka Scotland ibakie UingerezaPicha: picture-alliance/dpa/A. Rain

Scotland itapaswa kuunda Kamati yake ya kitaifa ya Olimpiki na kutambuliwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC. Shirikisho hilo jipya la Scotland kisha litahitaji kuwa na mafungamano na angalau mashirikisho matano ya michezo ulimwenguni. hilo siyo tatizo kwa Scotland. Lakini pia Scotland itahitaji kuidhinishwa rasmi na Umoja wa Mataifa kama taifa huru, na haijulikani hilo linaweza kuchukua muda gani. Naibu rais wa IOC Craig Reedie, ambaye ni raia wa Scotland, anasema itakuwa vigumu sana sana, kwa timu huru ya Olimpiki kuundwa kwa wakti unaofaa kabla ya michezo ya Rio. Rais wa IOC Thomas Bach anasema maslahi ya wanariadha wa Scotland yanaweza kutetewa kabla ya Michezo ya Rio, kama taifa hilo litajitenga.

Baadhi ya wanariadha wanaweza kuchagua kuiwakilisha Uingereza. Wascotland wanaweza kuamua kushinadana kama “wanariadha huru” chini ya bendera ya Olimpiki, kama ilivyofanyika katika miaka ya nyuma kwa wanariadha kutoka ule uliokuwa Muungano wa Kisovieti-yaani Urusi ya zamani, iliyokuwa Yugoslavia, Timor Mashariki na Sudan Kusini.

Maswali mengine muhimu kabla ya Rio ni: ni vipi wanariadha wa Scotland wanavyoweza kushiriki katika mchakato wa kufuzu kwa michezo ya Olimpiki? Timu ya Uingereza inaweza kuwachagua wanariadha wa Scotland kwa wakati huo? Nini kitafanyika kwa ufadhili wanaopata wanariadha wa Scotland kutoka mfuko wa michezo wa kitaifa wa Uingereza? Maswali hayo yataweza tu kujibiwa kwa kina baada ya wapiga kura kufanya uamuzi wao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu