1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye Biden na Netanyahu wazungumza

18 Februari 2021

Rais Joe Biden wa Marekani amezungumza kwa simu na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ikiwa ni mara ya kwanza kwa viongozi hao na kujadiliana kuhusu ushirikiano baina ya mataifa yao.

https://p.dw.com/p/3pVtX
Washington White House Oval Office Präsident Biden
Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Rais Joe Biden wa Marekani amezungumza kwa simu na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ikiwa ni mara ya kwanza kwa viongozi hao na kujadiliana kuhusu ushirikiano. Miongoni mwa masuala yaliyotiliwa umuhimu ni ushirikiano baina ya mataifa hayo na amani katika eneo la Mashariki ya Kati, hususan baina ya Israel na Palestina

Hata hivyo mazungumzo hayo hayakuonekana kuwa ya kawaida baada ya kusogezwa mbele kwa takriban mwezi mmoja, tofauti na huko nyuma ambapo viongozi wa mataifa hayo huzungumza katika kipindi cha siku chache baada ya kuingia madarakani.

Kusogezwa mbele kwa mazungumzo hayo kuliibua madai kwamba Biden alikuwa akikwepa kuzungumza na Netanyahu, na hasa kutokana na ukaribu aliokuwa nao waziri mkuu huyo na mtangulizi wa Biden, Donald Trump. Mapema wiki hii, msemaji wa ikulu ya White House Jen Psaki aliwaambia waandishi wa habari kwamba mazungumzo hayo yangali karibu mno.

Alisema, "Ngoja nianze kwa kuwathibitishia kwamba simu yake ya kwanza na viongozi wa kikanda ni ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu. Itakuwa hivi karibuni. Mnajua, Israel ni mshirika wetu."

Biden asifu mazungumzo.

 Israel Anhörung im Korruptionsprozess Regierungschef Netanjahu
Waziri mkuu Benjamin Netanyahu alikuwa na mahusiano mazuri na Donald Trump, hali iliyozua wasiwasi kuhusiana na mahusiano yake na BidenPicha: Reuven Castro/AP/dpa/picture alliance

Baada ya mazungumzo hayo ya jana, Biden aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter, kwamba wamekuwa na mazungumzo ya karibu saa moja yaliyokuwa ya kirafiki na yaliyojaa ucheshi, akisema wamekubaliana kuimarisha ushirikiano baina yao.

Kulingana na Ikulu ya White House, Biden alitilia mkazo namna atakavyoendelea kuunga mkono makubaliano ya kurejesha mahusiano kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu na Kiislamu katika hali ya kawaida, yaliyosimamiwa na serikali ya Trump. Aidha alisisitizia kuhusu umuhimu wa kusaka amani ya kikanda hususan kati ya Israel na Palestina.

Wiki iliyopita balozi wa zamani wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa Danny Danon alimuomba Biden kumpigia simu Netanyahu, na kuorodhesha kupitia ukurasa wake wa twitter mataifa kumi ambayo tayari wakuu wake wamezungumza na Biden. Netanyahu alikuwa ni swahiba mkubwa wa Trump, tofauti na mtangulizi wa Trump, Barack Obama, ambaye Biden alikuwa makamu wake. 

Ofisi ya Netanyahu ambayo ilikuwa ya kwanza kutangaza mazungumzo hayo, ilichapisha picha iliyomuonyesha waziri mkuu huyo akitabasamu huku akiwa ameshikilia simu. Hata hivyo haikuzungumzia kwa kina kuhusiana na mazungumzo ya wakuu hao.

Kitisho cha Iran, moja ya ajenda muhimu.

Masuala mengine yaliyopewa kipaumbele kulingana na ofisi ya Netanyahu yalikuwa kuhusu kitisho cha Iran kufuatia hatua yake ya kutengeneza silaha za nyuklia na juhudi zao katika kupambana na janga la virusi vya corona.

USA Washington Weißes Haus | Abkommen Naher Osten
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Donald Trump baada ya kusaini makubaliano ya AbrahamPicha: Reuters/T. Brenner

Netanyahu anajivunia mahusiano yake na marais wa mshirika wake wa karibu kabisa Marekani pamoja na wakuu wa mataifa mengine. Pamoja na masuala mengine, waziri mkuu huyo anatarajia kumzuia Biden kurejea kwenye makubaliano ya nyuklia na Iran ambayo Israel inayapinga vikali.

Biden amekuwa akijizuia kuzungumza na Netanyahu kwa sehemu ni kwa sababu kwanza alitaka kuzungumza na washirika wake wakubwa wa Ulaya, wakati akiangazia hatua inayofuata na Iran, hii ikiwa ni kulingana na afisa mwandamizi aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa.

Waisrael wengi wanahofu kwamba Biden, aliyehudumu na Obama kama makamu wa rais, atafufua mpango wake kuelekea ukanda wa Mashariki ya Kati kwanza kwa kurejea kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran na pili kushinikiza makubaliano kati ya Israel na Palestina.

Soma Zaidi: Mpango wa Trump kuhusu Mashariki ya Kati: Dunia yatoa maoni 

Kwenye kampeni zake za urais, Biden alikosoa uamuzi wa Trump wa kujiondoa kwenye makubaliano hayo na Iran ya mwaka 2015. Lakini akiwa rais, ameisisitiza waziwazi Iran kutekeleza wajibu wake ulio chini ya makubaliano hayo, kabla serikali yake haijaanza kuangazia uwezekano wa kuviondoa vikwazo vilivyowekwa na serikali ya Trump.

Mashirika: DPAE/AFPE