Hakutakuwa na uchaguzi mpya asema rais wa Lukashenko
17 Agosti 2020Lukashenko amenukuliwa na shirika la habari la Belta, akisema isitarajiwe kamwe, kwamba anaweza kulazimishwa kufanya uamuzi chini ya shinikizo. Mwanasiasa wa upinzani nchini Belarus Sviatlana Tsikhanouskaya amesema leo kwamba yuko tayari kuiongoza nchi hiyo na kutoa wito wa kuundwa kwa mifumo ya kisheria kuhakikisha kwamba uchaguzi mpya wa urais unaandaliwa kwa njia huru.
Tsikhanouskaya ameongeza kwamba yuko tayari kuchukuwa jukumu la uongozi kwa wakati huu ili taifa liweze kurejelea hali yake ya kawaida, wafungwa wote wa kisiasa kuachiwa huru na kutayarisha mifumo ya kisheria na matakwa ya kuandaa uchaguzi mwingine wa urais katika muda mfupi uwezekanavyo na kwa njia huru na haki ambayo itakubaliwa bila maswali kutoka kwa jamii ya kimataifa.
Akizungumza kwa njia ya video akiwa nchini Lithuania, Tsikhanouskaya pia aliwahimiza maafisa wa usalama na sheria kujiondoa kutoka upande wa serikali ya rais Lukashenko na kuongeza kwamba mienendo yao iliyopita itasamehewa iwapo watachukua hatua hiyo sasa.
Wakati huohuo Uingereza imesema leo kuwa haitatambua matokeo ya uchaguzi huo wa Belarus uliowezesha kuchaguliwa tena kwa rais Lukashenko na kutoa wito wa uchunguzi huru katika matokeo hayo yanayokumbwa na utata.
Taarifa kutoka ikulu ya rais nchini Urusi hapo jana ilisema kuwa rais wa nchi hiyo Vladimir Putin alimwambia Lukashenko kuwa Urusi iko tayari kuisaidia Belarus kwa mujibu wa mkaba wa pamoja wa kijeshi iwapo itahitajika na kwamba shinikizo la nje linaelekezwa kwa taifa hilo japo haikubainishwa zinapotokea. Urusi inafuatilia kwa karibu huku Belarus ikisimamia mabomba yanayosafirisha kawi ya Urusi kuelekea mataifa ya Magharibi na hatua hiyo inaonekana na Urusi kama eneo la kinga dhidi ya jumuiya ya kujihami ya NATO.
Hii leo pia rais wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier amelihimiza jeshi la Belarus kutotumia ghasia huku raia wa nchi hiyo wakifanya maandamano kupinga matokeo ya uchaguzi ambayo kwa mara nyingine yamempa ushindi rais Lukashenko. Wakosoaji wanasema mchakato wa uchaguzi huo ulijaa udanganyifu.
Rais Steinmeier aliyesema kuwa anapendezwa na ujasiri wa waandamanaji hao, alimhimiza rais Lukashenko kupanga kuzungumza nao na kwamba watu wa taifa hilo wanastahili umoja na usaidizi.