1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lukashenko aonya kuchukua hatua kali dhidi ya waandamanaji

Sekione Kitojo
10 Agosti 2020

(Kiongozi wa kiimla wa Belarus Alexander Lukashenko ameonya kuwa maandamano ya wapinzani wanaopinga matokeo rasmi ya  uchaguzi yanayoelekea kurefusha utawala wake wa miaka 26 watakabiliwa na ukandamizaji mkubwa.

https://p.dw.com/p/3gkd7
Belarus Protest nach Präsidentenwahl in Minsk
Picha: picture-alliance/AP Photo

Lukashenko aliwaeleza  waandamanaji kuwa ni kama kondoo wanaotumiwa na mabwana zao kutoka  nje. 

Watu kadhaa  wamejeruhiwa  na  maelfu  wamekamatwa  saa kadhaa  baada  ya  uchaguzi  uliofanyika  jana  Jumapili, wakati polisi walipovunja  kikatili  maandamano  ambayo  wengi  walioshiriki walikuwa  ni  vijana kwa kutumia  mabomu  ya  kutoa  machozi na maguruneti ya kushitua. Wanaharakati  wa  makundi  ya  haki  za binadamu  wamesema  mtu mmoja  alifariki baada  ya  kukanyagwa na  gari ya  polisi, kitu  ambacho  maafisa  hao  wamekana.

Weißrussland Präsidentschaftswahlen Proteste und Ausschreitungen in Minsk
Waandamanaji wakitawanywa na polisi kwa kutumia mabomu ya kutoa machoziPicha: picture-alliance/dpa/S. Grits

Maafisa  wa  uchaguzi  wamesema  jana  kuwa  Lukashenko ameshinda muhula wa  sita  madarakani  kwa  asilimia 80 ya kura, wakati  mgombea  wa  upinzani Sviatlana Tsikhanouskaya amepata asilimia  9.9. Tsikhanouskaya ameyakataa  matokeo  hayo  rasmi kuwa ni udanganyifu na  kuapa kupambana kupinga  matokeo hayo, na upinzani  unapanga  maandamano  mapya  katika  mji  mkuu Minsk, pamoja  na  miji  mingine baadaye leo. Tsikhanouskaya amesema.

"Kile  kilichotokea  jana ni makosa ya serikali. Tumewaomba wasitumie nguvu dhidi  ya  watu ambao  wameingia  mitaani. Inauma. Na leo tumewafahamisha  kwamba  mtu mmoja  amefariki, lakini kwa sababu  hatuna  intaneti, hatuwezi kuthibitisha ama  kukataa. Nina matumaini sio kweli na  wote wako salama."

Weißrussland Präsidentschaftswahlen Proteste und Ausschreitungen in Minsk
Polisi wakiwakamata waandamanaji mjini MinskPicha: picture-alliance/dpa/S. Grits

Ukandamizaji wa kikatili

Ukandamizaji  huo  wa  kikatili  wa  polisi umesababisha  ukosoaji mkubwa  kutoka  mataifa  ya  Ulaya  na bila  shaka  utasababisha hali  tata  ya  juhudi  za  Lukashenko  kuweka  mahusiano  mazuri  na mataifa  ya  magharibi  mnamo  wakati kuna  hali  ya  wasiwasi  na mshirika wake  wa  karibu  na  mfadhili, Urusi.

Lakini  Lukashenko , ambaye utawala wake wa mkono  wa  chuma wa  miaka  26 umesababisha hali ya kutokuridhika  katika  taifa  hilo la  iliyokuwa umoja  wa  kisovieti  lenye  wakaazi  milioni 9.5, ameonya  kuwa  hatasita  kutumia  nguvu  tena  kuyatawanya maandamano  ya  wapinzani. Amedai  kuwa  waandamanaji walikumbana  na  jibu  sahihi  usiku  baada ya  kuwajeruhi  maafisa 25 wa polisi  na  kujaribu  kuchukua  udhibiti wa  majengo  ya  serikali katika  miji  kadhaa  ya  Belarus.

Belarus Präsidentschaftswahl Oppositionskandidatin Swetlana Tichanowskaja
Mgombea wa upinzani Svetlana TichanowskayaPicha: Reuters/V. Fedosenko

"Hatutawaruhusu  kuivuruga  nchi  yetu ," amesema. "tulitaka kuifanya  siku hii  kuwa ni ya  mapumziko  kwa  watu. lakini  baadhi walitaka kuharibu  siku  ya  mapumziko."

Mkurugenzi  huyo  wa  zamani  wa  mashamba  ya  serikali  mwenye umri  wa  miaka  65 amedokeza  kwamba  upinzani  unaongozwa kutokea  Poland  na  Jamhuri  ya  Cheki, na  kuongeza  kuwa  baadhi ya  makundi  nchini  Ukraine  na  Urusi  huenda  pia  yalikuwa  nyuma ya  maandamano  hayo.