1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres: Dunia ichukue mtazamo wa kivita dhidi ya Covid-19

Daniel Gakuba
24 Mei 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezihimiza serikali za mataifa ya dunia kutumia mbinu za wakati wa vita, kuondoa mwanya uliopo kati ya nchi tajiri na masikini katika kushughulikia janga la Covid-19.

https://p.dw.com/p/3tsi3
Deutschland UN-Generalsekretär Guterres im Bundestag
Picha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

 Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa Shirika la Afya ulimwenguni WHO unaofanyika mjini Geneva leo, Guterres  mbinu hizo zisipotumiwa, kitakachofuata ni nchi tajiri kuwapa chanjo watu wao na kuzingua shughuli za kiuchumi, huku zile maskini zikisalia katika mzunguko wa maambukizi.

Mkutano huo wa WHO mjini Geneva unafanyika wakati nchi kama India na Brazil zikishuhudia ongezeko la vifo vinavyosababishwa na Covid-19, wakati kasi ya maambukizi na vifo kama hivyo vikishuka katika mataifa yenye uchumi imara kama Marekani, Uingereza na Israel.

Soma zaidi: Kuanzia Juni 7 chanjo kwa wote Ujerumani

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema dunia inapaswa kuchukua mtazamo wa wakati wa vita, na kutumia silaha ya chanjo kupambana na janga la virusi vya corona.

Huenda idadi hali ya vifo vya Covid-19 ni kubwa kuliko inayojulikana

Weltspiegel 7.7.21 | Indien Corona-Situation Garhmukteshwar
India imekuwa ikishuhudia idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na Covid-19Picha: Danish Siddiqui/REUTERS

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa tayari watu milioni 3.4 wamekufa kutokana na Covid-19, lakini wataalamu wanasema idadi halisi ni kubwa zaidi kuliko hiyo. Profesa Gautam Menon, mkufunzi wa bailojia katika chuo kikuu cha Ashoka nchini India anatoa mfano, akisema maiti za wahanga wa janga hilo zilizotapakaa kando ya mto Ganges hazijaorodheshwa katika takwimu za waliopoteza maisha kutokana na virusi vya corona.

Soma zaidi: Hali ya Covid-19 bado ni tete India

Akizungumza katika mkutano huo huo, Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema angependa kuona angalau asilimia 10 ya watu wa kila taifa duniani wakiwa wamepatiwa chanjo ya Covid-19 ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu.

Merkel apendekeza mkataba wa kimataifa kwa ajili ya majanga

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pia ameuhutubia mkutano huo, na kutoa rai ya kusainiwa mkataba wa kimataifa juu ya utayarifu wa kuzuia majanga.

3. Ökumenische Kirchentag 2021
Angela Merkel, Kansela wa UjerumaniPicha: oekt.de

''Janga moja linapomalizika, janga jingine linakuja. Tunapaswa kuwa tayari iwezekanavyo kupambana na janga linalofuata. Huo ndio ujumbe ambao ningependa kuusikia kutoka mkutano huu,'' amesema Kansela Merkel.

Pendekezo hilo la Kansela Merkel limeungwa mkono na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, aliyetaka shirika la afya ulimwenguni liimarishwe kwa kupatiwa uwezo wa kukabiliana na janga pale tu linapojitokeza.

Katika hotuba yake Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhenom Ghebreyesus amewakumbuka kwa hali ya kipekee wahudumu wa afya 115,000 waliokufa tangu kuibuka kwa virusi vya corona, akisema walijitolea maisha yao kuwasaidia watu wengine kuendelea kuishi.

Tedros amesikitishwa na namna chanjo zinavyosambazwa duniani, akisema dozi zilizongenezwa zingeweza kuwanusuru wahudumu wote wa afya kama zingetolewa kwa usawa, akisema zaidi ya asilimia 75 ya dozi za chanjo ya Covid-19 zilizokwishatengenezwa zimeelekezwa katika matiafa 10 duniani.

afpe, rtre