Goodluck Jonathan aongoza uchaguzi Nigeria
18 Aprili 2011Nigeria imeweza kuendesha kwa mafanikio zoezi la uchaguzi wa rais hapo Jumamosi baada ya kufanikisha uchaguzi wa bunge hapo tarehe 9 mwezi huu. Waangalizi wa uchaguzi huo pamoja na wapiga kura wengi wameonyesha kuridhishwa na hali inayoendelea ya amani na utulivu katika zoezi hili la uchaguzi na jinsi ulivyotayarishwa.
Rais Goodluck Jonathan anaongoza akiwa hadi sasa amepata kiasi cha kura milioni 22 zilizohesabiwa kutoka majimbo 35 kati ya 36 nchini Nigeria.
Tume huru ya uchaguzi bado inasubiri matokeo kutoka katika jimbo moja pamoja na baadhi ya maeneo. Chama cha rais Jonathan cha Peoples Democratic Party, PDP, kimepata kura nyingi katika maeneo ya kusini ambako ndiko anakotoka pamoja na kusini magharibi , kusini mashariki na kaskazini kati.
Idadi kubwa ya wapigakura milioni 73.5 ambao wamejiandikisha kupiga kura walijitokeza siku ya Jumamosi katika uchaguzi huo wa rais.
Mpinzani mkuu wa Jonathan, kiongozi wa zamani wa kijeshi Muhammadu Buhari, amepata hadi sasa kura milioni 10.8 kutoka katika eneo la kaskazini ambako ni ngome yake. Mgombea kijana zaidi kati ya wagombea watatu wa kiti cha urais, Nuhu Ribadu wa chama cha Action Congress of Nigeria ACN, amepata kura milioni 2.2.
Buhari ambaye amegombea kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Congress for Change, amesema kuwa hatapinga matokeo ya uchaguzi mahakamani, lakini chama chake kinaweza kufanya hivyo iwapo kitapenda.
Aligombea akashindwa katika uchaguzi wa mwaka 2003 na 2007 dhidi ya chama tawala cha Peoples Democratic, PDP.
Kushindwa kwa ushirika baina ya chama cha CPC na Action Congress of Nigeria ACN kumesababisha Jonathan kushinda katika eneo la kusini magharibi ya Nigeria, kufuatia mashauriano ya muda mrefu na wadau ili wamuunge mkono. Muungano wa chama cha CPC na ANC ulishindikana kutokana na madai ya masharti ambayo hayakuweza kukubalika kwa pande zote . Ulinzi uliongezwa katika kituo cha kupokea matokeo mjini Abuja , mji mkuu wa nchi hiyo, ambapo viongozi wa idara mbali mbali za vyuo vikuu walitumika kama maafisa wa kutuma taarifa za matokeo kutoka katika majimbo 36 na miji mikuu ya majimbo, ambapo huo ni utaratibu mpya ambao unatarajiwa kuleta hali ya kuaminika na kuhakikisha uwazi wa zoezi la uchaguzi. Mkuu wa ujumbe wa waangalizi kutoka umoja wa Ulaya , Alojz Peterle ameusifu uchaguzi huo siku ya Jumamosi, na siku moja baadaye kundi la waangalizi wa ndani wa Nigeria pia lilifanya hivyo. Mradi wa hesabu ya haraka , 2011 Swift Count, ulituma wawakilishi karibu 1,500 katika uchaguzi wa majimbo. Wakili Dafe Akpedeye alitoa matokeo ya kundi la mradi huo mjini Abuja.
Mradi wa hesabu ya haraka umeweza kufanyakazi katika nchi nzima, na kuwezesha kuwapa fursa halisi wananchi kuweza kutimiza haki yao ya kushiriki katika zoezi hili. Hatua za uchaguzi zilikwenda vizuri kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa bunge wiki moja kabla.
Hata hivyo ghasia za hapa na pale zimetokea katika sehemu za kaskazini za Nigeria usiku wa kuamkia leo wakati rais Goodluck Jonathan akielekea kupata ushindi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais, wameeleza polisi na wakaazi wa eneo hilo. Madai ya wizi wa kura yamesababisha ghasia mitaani katika baadhi ya sehemu za majimbo ya Kaduna na Sokoto. Hapo mapema majumba yalichomwa moto katika jimbo la Bauchi na Gombe.
Mwandishi : Thomas Mösch / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman