GMF: Kuchangiana Masuluhisho dunia inapokabiliwa na migogo
17 Juni 2024Washiriki zaidi ya 1,500, wazungumzaji zaidi ya 160, kutoka nchi zaidi ya 100 ndani ya siku mbili hapa kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano mjini Bonn.
Wote wanajaribu kusaka njia za kushirikiana kukabiliana na ulimwengu unaozama kwa kasi kwenye migogoro, iwe ya vita, mabadiliko ya tabianchi na, kwa siku za karibuni, teknolojia mpya ya akili ya kubuni, ama kama waiitavyo wengine, akili mnemba.
Katikati ya migogoro hiyo, ni jukumu la wanahabari kuunganisha baina ya makundi mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kijinsia, ili kuufanya ulimwengu kuwa mahala salama kwa kuishi kwa kila mmoja.
Soma pia:Kongamano la vyombo vya habari la DW kuangazia usumbufu na ubunifu
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Annalena Bearbock, amesema kwenye hotuba yake kwa washiriki kwamba hiyo ndiyo nguvu ya vyombo vya habari:
"Nguvu kubwa kabisa ya uandishi wa habari, ya nyinyi nyote muliopo hapa leo, ni uwezo wa kusimulia hadithi ambazo kama si nyinyi kamwe zisingejuilikana, kuuliza maswali ambayo kama si nyinyi kamwe yasingejibiwa, kuwawajibisha wale ambao nguvu zao kama si nyinyi huwa hazihojiwi, na kuwapa sauti wale ambao kama si nyinyi wasingesikika."
Uwandishi wa habari wenye kuleta matokeo
Mbali ya maudhui makuu ya Kuchangiana Masululisho, ambayo lengo lake ni kukusanya mawazo ya kila mmoja kwenye kutatua matatizo yanayotukabili, kongamano hili pia linajadili kile kinachoitwa uandishi habari wa kujenga, mbinu za kuripoti kwenye maeneo ya migogoro mikubwa ya kisiasa na kijamii, na pia nafasi ya teknolojia ya akili ya kubuni, ambayo kwa sasa inakuwa kwa kasi kwenye ulimwengu wa mawasiliano.
Antony Diallo ni mdau wa tasnia ya habari na mwanasiasa wa siku nyingi nchini Tanzania, ambaye ana wasiwasi na jinsi ambavyo teknolojia hiyo inavyotumika kwenye vyombo vya habari:
Kongamano hili ni fursa ya wanahabari kukutana kutoka pande mbalimbali ulimwenguni, kuanzisha mawasiliano na kubadilishana uzoefu kwenye taaluma yao.
Soma pia:Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari laanza Bonn
Ndio maana mbali ya waandishi wakubwa wa kimataifa, Deutsche Welle huwaalika pia waandishi kutoka jamii za pembezoni, na makundi yasiyo na sauti, kama vile wakimbizi.
Nira Ismail, mwanahabari kutokea kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya, mwenyewe akiwa mkimbizi kutokea Sudan
"Hakuna haja ya mwandishi kutoka taifa jingine aje kuzungumza kwa niaba yetu laah! Wenyewe tunaweza kujizungumzia na kupata masuluhisho."
Kongamano linaendelea na kumalizika kesho, ambapo washiriki wanatarajiwa kuendeleza mjadala mzito ulioanzia leo juu ya dhima ya vyombo vya habari vya mataifa ya kusini, yaani mataifa masikini, yanayolalamika kuwa hadithi yake inasimuliwa vibaya na vyombo vya habari vya kaskazini, kwa maana ya mataifa tajiri.