Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari laanza Bonn
19 Juni 2017Kauli mbiu ya kongamano la mwaka huu ni "Utambulisho na Mchanganyiko". Katika hotuba yake ya ufunguzi mkurugenzi mkuu wa shirika la utangazaji la Deutsche Welle Peter Limbourg amesema kongamano hilo la siku tatu linatoa fursa ya kuangalia nyuma hatua zilizopingwa baada ya kikao cha kwanza kama hicho miaka kumi iliyopita hapa mjini Bonn. Limbourg amesema wakati huo hakukuwepo na changamoto chungu nzima kama zinazoshuhudiwa hivi sasa kwani wakati wa kufanyika kikao hicho kulikuwepo utulivu maeneo mbalimbali ulimwenguni, hakukuwepo na mgogoro wa kifedha, umwangikaji damu hasa mataifa mengi mataifa ya kiarabu, hakukuwepo na idadi kubwa ya wakimbizi wanaohamia bara la Ulaya, vita vya Ukraine havikuwepo, Donald Trump alikuwa tu na kipindi cha televisheni na ni idadi chache tu ya Waingereza waliokuwa na ndoto ya kujitoa kutoka kwa Umoja wa Ulaya, Brexit.
Limboung amesema nyakati hizi kuna misukosuko zaidi ambayo inaathiri utendakazi wa waandishi wa habari na hasa vyombo vya kimataifa vya utangazaji. "Kuna uwiano wa moja kwa moja kati ya kiwango cha ukandamizaji wa kitaifa na matumizi ya vyombo vya kimataifa vya utangazaji," mkuu wa DW aliuambia mkutano huo. Watangazaji wanaonekana kuwa wa kuaminika ndio wanaonufaika.
Kuenea kwa taarifa za kupotosha
"Mwaka huu washiriki wa kikao hicho wanaangazia mfumo wa dijitali katika sehemu za kazi," Mkurugenzi wa kongamano hilo la Global Media Forum Patrick Leush alisema. Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa uandishi habari unakabiliwa na changamoto kubwa ambapo kila mtu anaweza kutoa habari na kupokea, na hali hiyo inafanya kuwa vigumu kwa vyombo vya habari kuaminika. Uaminifu wa vyombo vya habari ni suala lililopewa kipaumbele na washiriki katika kongomano hili na litaendelea kujitokeza kadri mjadala unavyoendelea kutokana na kuenea taarifa za upotoshaji.
Kongamano hilo linahudhuriwa na karibu washiriki elfu 2 kutoka mataifa 130. Kando na waandishi wa habari kutoka Afrika washiriki wengine ni pamoja na wanasisa kutoka hapa Ujerumani, shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, miongoni mwa mashirika mengine.
Tuzo ya uhuru wa kujieleza - Freedom of speech award - mwaka huu inaenda kwa washirika wa vyombo vya habari wa ikulu ya Marekani. Mkurugenzi mkuu wa Deutsche Welle Peter Limbourg amesema uhuru wa kujieleza unapaswa kulindwa ulimwenguni kote kwa sababu ni nguzo muhimu ya demokrasia.
Mwandishi:Jane Nyingi /Matthias von Hein (db)
Mhariri:Josephat Charo