EU yamwaga waangalizi wa Uchaguzi Tanzania
29 Oktoba 2010Timu hiyo ya waangalizi inaongozwa na mbunge katika Bunge la Ulaya, Bwana David Martin, na itakuwepo nchini Tanzania hadi kumalizika kwa uchaguzi huo. Wengi wa waangalizi kwenye timu hiyo ni watu waliokwishafanya kazi hii kwa miaka mingi katika nchi kadhaa ulimwenguni, na Umoja wa Ulaya umepanga kuwasambaza katika kila kona ya nchi kufuatilia namna uchaguzi huu unavyoendeshwa.
Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani leo hii (13 Oktoba 2010), Bwana Martin amesema kwamba Umoja wa Ulaya unasisitiza msingi wake wa uangalizi kwamba timu yake haina upendeleo wa chama chochote cha siasa wala mgombea wa nafasi yoyote ya uongozi, isipokuwa ipo kuangalia namna vyombo vinavyohusika na uchaguzi vinavyosimamia wajibu wake na katika mazingira gani uchaguzi huu unafanyika.
Timu hii ya waangalizi imejigawa katika makundi mawili, ambapo kuna wale ambao wapo nchini Tanzania kwa muda mrefu na wale ambao watakuwepo kwa muda mfupi. Tayari waangalizi wa muda mrefu wapo nchini Tanzania tangu kuanza kwa kampeni karibuni miezi miwili iliyopita na wamekuwa wakirikodi na kuwasilisha ripoti zao kwa Ofisi Kuu ya Uangalizi iliyopo Dar es Salaam. Kwa mujibu wa Bwana Martin, waangalizi wa muda mfupi wanatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kiasi ya wiki moja kabla ya upigaji kura.
Kinyume na ilivyokuwa kwa chaguzi zilizopita, safari hii Umoja wa Ulaya inapeleka waangalizi wake katika maeneo karibuni yote ya nchi, hatua inayochukuliwa kama dalili ya kuimarika kwa umakini wa Umoja huo katika kufuatilia siasa za Tanzania.
"Waangalizi wetu watasambaa nchi nzima. Dar es Salaam, Zanzibr, Pemba, Kilimanjaro, Arusha. Wakwenda nchi nzima." Amesema Bwana Martin.
Kuhusiana na hali ya Zanzibar, ambayo ilizoeleka kuwa na matatizo ya uvunjaji wa amani katika siku hizi za uchaguzi, Bwana Martin amesema kwamba Umoja wa Ulaya umetiwa moyo sana na maendeleo ya kisiasa yaliyoko visiwani huko ambayo yamesababishwa na maridhiano ya kisiasa kati ya Chama cha Mapinduzi, CCM, na Chama cha Wananchi, CUF.
Umoja wa Ulaya pia umetiwa moyo na utendaji wa Tume zote mbili za Uchaguzi nchini Tanzania, yaani ile Taifa, NEC, na ile ya Zanzibar, ZEC. Bwana Martin amesema kwamba kiwango cha ufanisi wa tume hizo kinatia matumaini kwamba vyombo hivi vitawajibika vyema katika uchaguzi ujao.
"Nilikuwepo Zanzibar hivi karibuni na nimeiwa moyo sana na hali ya huko. Vyama vinafanya kampeni zake kwa utulivu na tume ya uchaguzi ya Zanzibar inaonekana kujitayarisha vyema zaidi safari hii," Bwana Martin amesema.
Tanzania, ambayo ni nchi ya Muungano wenye pande mbili, inafanya uchaguzi wake wa nne wa vyama vingi tangu kurudishwa tena kwa mfumo huu hapo mwaka 1992. Katika chaguzi zilizotangulia, hasa kwa upande wa Zanzibar, kulikuwa kukiripotiwa matukio ya uvunjaji wa haki za binaadamu mara kwa mara, jambo ambalo mara nyingi lilizifanya nchi za Umoja wa Ulaya kuwapa tahadhari raia wao wanaotembelea visiwa hivyo maarufu kwa utalii.
Lakini katika uchaguzi wa mara hii, kile kinachoitwa maridhiano ya kisiasa yaliyotokana na mazungumzo baina ya Rais anayemaliza muda wake, Amani Karume, na mgombea wa sasa Urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kimeitulizanisha hali na hivyo kujenga matumaini mapya si kwa waangalizi tu, bali hata kwa wananchi wenyewe. Umoja wa Ulaya ni mfadhili mkubwa wa shughuli za maendeleo nchini Tanzania, zikiwemo shughuli za kuimarisha demokrasia kama hili zoezi la uchaguzi.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo