Ushirikiano wa aina mpya kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya
28 Septemba 2010Mkutano wa ngazi ya juu uliopewa jina "Ushirikiano Afrika" umefungua ukurasa mpya katika ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika,na pia kati ya nchi za Afrika wenyewe kwa wenyewe.Hata mageuzi katika siasa ya maendeleo ambayo yanahusika zaidi na tija badala ya kiwango,yamejadiliwa.
Mnamo wakati huu tulio nao,"Machofu ya wafadhili" ndio usemi ulioingia sana midomoni .Lengo la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Milenia ,kutenga angalao asili mia sifuri nukta sabaa ya pato la ndani kwaajili ya misaada ya maendeleo limefuatwa na nchi chache tu tajiri kwa viwanda.Hoja inayotolewa mara nyingi ni bajeti dhaifu,lakini pia hali ya kukata tamaa kwamba miongo kadhaa ya misaada ya maendeleo haijasaidia kuupiga vita umaskini katika nchi zinazofadhiliwa.Kamishna wa Umoja wa Ulaya anaesimamia misaada ya maendeleo Andris Piebalgs anadhibitisha hoja hizo na kusema:
"Misaada pekee haitoshi ikiwa hatutojishughulisha na kiini cha hali hiyo.Bila ya kuheshimiwa sheria,bila ya usalama na bila ya kuwepo uwazi katika matumizi ya fedha za serikali,msaada hauwezi hata kidogo kuwapatia wananchi faida ya muda mrefu."
Mnamo miaka ya hivi karibuni bara la Afrika limekua likijivunia ukuaji mkubwa ajabu wa kiuchumi.Hali hiyo ilizipa matumaini nchi nyingi za Afrika kuweza kujikomboa wenyewe na kujitoa kutoka janga la umaskini.Mark Plant wa shirika la fedha la kimataifa anasisitita hali hiyo haizihusu nchi zote za Afrika.Anatilia mkazo amani,tangu ya ndani nchini mpaka kufikia amani pamoja na majirani.Mark Plant anasema ni jukumu la mashirika ya kimataifa kusaidia kutafuta ufumbuzi wa mizozo inayolikumba kila kwa mara bara la Afrika.
Kamishna wa masuala ya kiuchumi katika Umoja wa Afrika,Maxwell Mkwezalamba anasema:
"Ninaamini neema barani bAfrika itategemea jinsi nchi za Afrika zitakavyoshirikiana wenyewe kwa wenyewe na jinsi zitakavyoshirikiana na mataifa mengine."
Wajumbe wote mkutanoni wanakubaliana uhusiano kati ya Ulaya na Afrika umebadilika.Afrika inajiamini zaidi na ina nafasi ya kujikomboa wenyewe toka hali ya umaskini.Na pengine hali hiyo ndiyo itakayofungua njia ,kwa mara ya kwanza tangu uhuru ya kuwepo ushirikiano wa kweli kati ya pande hizi mbili .
Mwandishi:Hasselbach,Christoph (DW Brüssels)/Hamidou Oummilkheir
Mpitiaji:M.Abdul-Rahman