1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yaahidi Euro bilioni 1 kwa wakimbizi Mashariki ya Kati

24 Septemba 2015

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wameahidi kutoa euro bilioni 1 kusaidia wakimbizi katika nchi za Mashariki ya Kati katika juhudi za kuondoa tofauti zao juu ya namna ya kuutatua mzozo wa wahamiaji unaouzonga umoja huo.

https://p.dw.com/p/1GcEq
Mzozo wa wakimbizi umezua tofauti kimaoni miongoni mwa viongozi wa Ulaya
Mzozo wa wakimbizi umezua tofauti kimaoni miongoni mwa viongozi wa UlayaPicha: picture-alliance/AA

Msaada ambao ni miongoni mwa maazimio mengine yaliyofikiwa, umekubaliwa katika mkutano wa viongozi hao ambao umefanyika mjini Brussels usiku wa kuamkia leo. Maazimio hayo muhimu kuhusu namna ya kuushughulikia mzozo wa wahamiaji unaoendelea kugonga vichwa vya habari, yamefikiwa baada ya miezi kadhaa ya malumbano miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya.

Euro bilioni moja zitakazotolewa na Umoja wa Ulaya zitapitia katika mashirika ya msaada ya Umoja wa Mataifa, hususan lile la chakula, WFP, na la kushughulikia wakimbizi, UNHCR.

Akizungumza katika mkutano huo usiku wa kuamkia leo mjini Brussels, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema, ''Tunapokabiliwa na changamoto hii kubwa, Ulaya haiwezi kusema - Hapana, hatutaushughulikia-. Hilo litakuwa ni kosa kubwa''.

Hali mbaya makambini, sababu ya mmiminiko

Kansela Merkel amesema Umoja wa Ulaya umepuuzia upungufu wa fedha katika mashirika ya kimataifa ya msaada, na kwamba watu wanakufa njaa katika kambi za wakimbizi. Hali mbaya katika kambi hizo imechangia kuwafanya watu wafunge safari hatari za kuelekea Ulaya, na kusababisha mgogoro mkubwa wa wahamiaji unaoshuhudiwa hivi sasa. Kulingana na maoni yake, hatua iliyopigwa leo inatia moyo.

Hali mbaya ya maisha katika kambi za wakimbizi imechochea wengi kutaka kwenda Ulaya
Hali mbaya ya maisha katika kambi za wakimbizi imechochea wengi kutaka kwenda UlayaPicha: picture-alliance/AP Photo/Mohammed Zaatari

''Nimeridhishwa na matokeo ya leo, ingawa tunafahamu kuwa mahitaji yote kuelekea kwenye suluhisho la kudumu kwa mzozo wa wakimbizi hayajatimizwa. Tumepiga hatua muhimu mbele, na hii inadhihirisha kuwa ilikuwa muhimu kwa baraza hili kukutana kubadilishana mawazo, ili kupata uelewa sahihi wa tatizo hili.'' Amesema Bi Merkel.

Wengi wa wakimbizi milioni 1.3 wa Syria hivi sasa wanaishi kwa kutegemea senti hamsini za dola, amesema spika wa bunge la Ulaya Martin Schulz, ambaye pia amearifu kuwa kwa sasa mashirika ya msaada yanayo asilimia 40 tu ya kiwango cha fedha wanazohitaji kuendesha shughuli zao.

Kuta mipakani siyo jawabu

Viongozi wa Ulaya wamekubaliana pia kuendeleza mjadala na nchi zinazohifadhi idadi kubwa ya wakimbizi, ambazo ni Uturuki, Jordan na Lebanon, kuhusu masuala yanayohusu wakimbizi. Hata hivyo rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk, amesema hawatajihusisha na matakwa ya Uturuki ya kuweka eneo salama kaskazini mwa Syria dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu, akisema kwa sasa kipaumbele ni kutafuta ufumbuzi wa tatizo la wakimbizi wanaomiminika Ulaya.

Miezi ya hivi karibuni maelfu ya wakimbizi wamemiminika kwenye mipaka ya Umoja wa Ulaya
Miezi ya hivi karibuni maelfu ya wakimbizi wamemiminika kwenye mipaka ya Umoja wa UlayaPicha: picture-alliance/dpa/V. Gurgah

Kansela Angela Merkel amesema suluhisho la kudumu litafikiwa kwa kuzisaidia nchi watokako wakimbizi.

''Binafsi sidhani kuwa kujenga kuta kati ya nchi zetu ni suluhisho. Hatutaweza kulinda mipaka yetu bila kuishirikisha Uturuki, na kuunga mkono kuwepo serikali nchini Libya. Tutapata jibu kwa ushirikiano na washirika wetu. Lazima tufanye nao kazi pamoja.'' Amesema Kansela wa Ujerumani.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya hali kadhalika wameazimia kuimarisha ulinzi wa mipaka ya nje ya Umoja huo, na kusahihisha kile ambacho Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk amekiita ''Sera ya milango na madirisha vilivyo wazi''.

Awali viongozi hao waliidhinisha mpango wa kugawana wakimbizi 120,000 miongoni mwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya, ambao ulifikiwa na mawaziri wa mambo ya ndani, licha ya kupingwa na nchi kadhaa za Ulaya Mashariki.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/ape

Mhariri:Josephat Charo