1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji wamiminika Croatia

Admin.WagnerD17 Septemba 2015

Maelfu ya wakimbizi wameanza kumiminika nchini Croatia leo hii baada ya kurushiwa mabomu ya machozi nchini Hungary. Idadi ya wakimbizi hao walioingia Ujerumani jana pia imeripotiwa kuongezeka maradufu.

https://p.dw.com/p/1GXqP
Kroatien Serbien Flüchtlinge bei Tovarnik
Wahamiaji nchini CroatiaPicha: picture-alliance/AA/M. Ozturk

Maelfu ya wakimbizi wanamiminika nchini Croatia kama njia mpya ya kuingilia Ulaya ya magharibi baada ya kufukuzwa nchini Hungary kwa kurushiwa mabomu ya kutoa machozi pamoja na maji ya kuwasha. Polisi wa Croatia imesema wahamiaji 5,650 wameingia nchini humo leo hii, lakini kundi la mwanzo la wahamiaji lilianza kuingia nchini humo mapema jana. Mamlaka husika zimekuwa zikitumia mabasi pamoja na treni kuwasafirisha na kuwapeleka katika vituo vya wakimbizi.

Mamlaka nchini Croatia zimesema zinaunda bodi maalumu ya kukabiliana na umiminikaji huwo wa wakimbizi. Waziri wa mambo ya ndani Ranko Ostojic ameseme hadi sasa Croatia imeweza kuidhibiti hali hiyo ila alionya kuwa pale wimbi la wakimbizi kutokea Serbia litakapoanza kuingia nchini humo basi hatua mpya zitahitajika kutumika.

Hapa Ujerumani msemaji mkuu wa Polisi amesema leo idadi ya wahamiaji walioingia nchini tangu jana imeongezeka marudufu hadi kufikia watu 7,266. Naye kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema leo kuwa Ujerumani inazingati njia za kuwasaidia wahamiaji kuzoea maisha ya Kijerumani na maadili ya nchi:

Sondersitzung Merkel und die Ministerpräsidenten der Bundesländer
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (Katikati)Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa

"Bila shaka, maswali mengi yanapewa kipaumbele katika hatua hii. Idadi ya vitanda, usajili wa wahamiaji, na kadhalika. Na mamlaka za serikali ya shirikisho ya Ujerumani zimekubaliana kufanya kazi hii kwa pamoja. Lakini la muhimu ni mtazamo wa muda mrefu yaani ni kazi ya kuwajumuisha wahamiaji ndani ya mfumo wetu wa kijamii, na maadili ya nchi yetu kwa ujumla, kwa wale wanaokuja kukaa hapa kwa muda mrefu," alisema Merkel.

Denmark kutoshiriki mpango wa Ulaya wa wahamiaji

Naye kamishana wa Umoja wa Ulaya Dimitris Avramopoulus amesema ana imani kuwa mawaziri wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya watafikia makubaliano wiki ijayo, juu ya namna ya kugawana jukumu la kupokea wakimbizi barani Ulaya. Mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya watakutana tena Jumanne ijayo baada ya kushindwa kukubaliana juu ya pendekezo la tume ya Ulaya la kugawana wahamiaji 160,000 miongoni mwa nchi wanachama 28 wa umoja huwo kulingana na uwezo wa kiuchumi na idadi ya watu wa kila nchi.

Kwa upande wa Denmark, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Lars Loekke Rasmussen, amesema nchi yake imejitolea kupokea wahamiaji 1,000 katika kipindi hiki kisichokuwa cha kawaida, lakini haitashiriki katika mpango wowote utakaopangwa na Umoja wa Ulaya wa kupokea maelfu ya wahamiaji wanaomiminika barani humo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/ape/rtre

Mhariri: Gakuba Daniel