1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKosovo

EU: Viongozi wa Kosovo na Serbia watulize mvutano uliopo

30 Mei 2023

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amewatolea mwito viongozi wa Kosovo na Serbia kusitisha mvutano mara moja baada ya mapigano kutokea Kaskazini mwa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/4RyiG
EU l Hoher Vertreter der Union für Außen- und Sicherheitspolitik, EU-Kommision - Josep Borrell
Picha: Philipp von Ditfurth/dpa/picture alliance

Borrell amesema tayari ameshazungumza na Waziri Mkuu wa Kosovo Albin Kurti na rais wa Serbia Alexander Vucic kuwaambia wajiepushe na matamshi yanayoweza kuchochea hali kuwa mbaya zaidi. Amesema amewaomba viongozi wote wawili kuweka mikakati ya kutuliza mivutano iliopo.

Mkuu huyo wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema serikali ya Kosovo inahitaji kuondoa vikosi vya polisi katika majengo ya serikali za mitaa Kaskazini mwa Kosovo na waandamanaji wa kabila la Serb wanapaswa kuacha kuandamana, huku akionya kwamba Umoja wa Ulaya unajadili hatua zinazoweza kuchukuliwa iwapo pande husika zitaendelea kukataa hatua za kudhibiti hali.

Kabila la Serb linalochangia asilimia 6 ya idadi Jumla ya watu wa Kosovo lilisusia uchaguzi uliokuwa na utata wa serikali za mitaa uliofanyika mwezi uliyopita katika miji ya Kaskazini ambako linapatikana kwa wingi na kutoa nafasi kwa kabila la Albania kuchukua udhibiti wa mabaraza ya jiji licha ya idadi ndogo ya watu kushiriki uchaguzi huo. Waserbia wengi wanataka kuondolewa kwa vikosi vya polisi na ma meya wa kabila la Albania ambao hawawaoni kama wawakilishi wao.

Ghasia zilianza pale wa serbia walipojaribu kuingia kwa nguvu katika eneo la mji wa Zvecan, lakini wakazuwiwa na polisi wa Kosovo waliowarushia mabomu ya kutoa machozi. Wanajeshi wa kulinda amani wa Jumuiya ya kujihami NATO waliingilia kati kujaribu kuwatawanya waandamanaji lakini walirushiwa mawe na chupa na takriban wanajeshi 30 wa Jumuiya hiyo wakajeruhiwa.

Urusi yazionya nchi za Magharibi kuacha propaganda dhidi ya Serbia

Russland Aussenminister von Syrien, Türkei, Iran und Russland treffen sich in Moskau
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei LavrovPicha: Russian Foreign Ministry via REUTERS

Kosovo ilijitangaza kuwa Huru kutoka kwa Serbia mwaka 2008 lakini Serbia na washirika wale Beijing na Moscow wamekataa kutambua hilo. Wa Serbia walioko Kosovo wanabakiak uwa watiifu kwa taifa lao hasa upande wa Kaskazini walioko kwa wingi na kwa kawaida wanapinga hatua yoyote ya Kosovo kujaribu kuwadhibiti.

Huku hayo yakiarifiwa Jumuiya hiyo ya Nato imesema inawapeleka wanajeshi wake zaidi Kaskazini mwa Kosovo kufuatia ghasia zinazoendelea upande wa Kaskazini. Kamanda wa jeshi hilo Admirali Stuart B Munsch amesema hatua hiyo ni ya kuhakikisha kuwa Ujumbe wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO nchini Kosovo  - KFOR, inauwezo wa kutosha unaouhitaji ili kuimarisha usalama chini ya sheria ya Baraza la Uslama la Umoja wa Mataifa. Stuart amesema pande zote ni lazima zisitishe hatua zinazoweza kuvuruga amani.

Huku hayo yakiarifiwa Urusi imezitakan nchi za magharibi kusitisha propaganda inayodai inaendeleza katika mzozo uliopo. Wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi imesema nchi hizo zinapaswa kuacha kuwalaumu waandamanaji wa kabila la serbs kusababisha hali inayoshuhudiwa nchini Kosovo. Urusi imesema waserbs wanajaribu kupigania haki zao za msingi na uhuru wao kwa amani na bila silaha.

Chanzo: afp/ap/reuters