Eneo la turathi lashambuliwa Yemen
12 Juni 2015Mashambulizi ya anga ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia yaliyofanywa leo hii katika mjini mkuu wa Sanaa, yameuwa watu watano na kuharibu nyumba tatu katika eneo kongwe linalotambuliwa na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kama turathi ya dunia.
Kwa mujibu wa wakaazi wa eneo hilo, mashambulizi hayo inasemekana ni ya mwanzo, katika eneo hilo kongwe tangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo ya dhidi ya wanamgambo wa kihuthi mwisho wa mwezi wa Machi.
"Marubani wa kihalifu wanalenga wananchi wasio na silaha waliokuwa wamelala kwa amani. Wanasema kuwa wanlenga kambi za kijeshi, ziko wapi kambi hizo za kijeshi hapa? Yako wapi waguruneti? Mungu akijaali nasi tutashambulia katika mipaka yao, haraka iwezekanavyo,“ alisema Mohamed Qelala jamaa wa mmoja wa waathirka.
Saudi Arabia yakanusha kuhusika na shambulizi
Hata hivyo muungano huo unaongozwa na Saudi Arabia umekanusha kuhusika na mashambulizi hilo katika eneo kongwe la kihistoria la mji mkuu wa Sanaa. Msemaji Mkuu wa muungano huo Jenerali Ahmed al-Assiri ameliambia shirika la habari la AFP na hapa ninamnukuu “ Kwa hakika hatuhusiki na mashambulizi hili ndani ya mji.”
Eneo hilo ambalo litatambuliwa na shirika la UNESCOkama turathi ya dunia limekuwa ni makaazi ya watu kwa miaka 2,500 sasa na Assiri amesma “ tunatambua kama maeneo kama haya ni mihimu sana.” Ameengeza kwa kusema waasi wanaweza wakawa wameficha silaha na risasi katika eneo hilo.
"Siku kadhaa kabla walikuwa na mripuko katika maeneo yao ya kuficha silaha" akiwazungumzia waasi wa kihuthi. "kwahio inaweza ikawa ni moja ya hayo." Assiri amesema pia marubani wa muungano huo huwa hawashambulii makaazi ya raia.
Mwandishi habari wa shirika la AFP amesema shambulizi hilo la kombora liliangukia katika mtaa wa Qassimi, ambao una maelfu ya majengo yaliyojengwa tangu karne ya 11.
Madaktari na waliyoshuhudia wamesema, ingawa kombora hilo halikuripuka lakini liliharibu majengo matatu ya kizamani na kuuwa watu watano, ikiwamo mwanamkwe mmoja na mtoto.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la UNESCO Irina Bokova amesema amesikitishwa sana na vifo vya watu hawa pamoja na majengo yaliyoharibiwa ambayo ni johari za zamani kabisa za ujenzi wa Kiislamu. Alisema pia uharibifu huu utachochoea hali mbaya ya kibinaadamu iliyoko na anazisisitiza pande zote kuheshimu na kulinda turathi za tamaduni za Yemen.
Mkutano wa Geneva
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Ismail Ould Ahmed amesema ataitisha mazungumzo tafauti na pande zote mbili zinazozozana mjini Geneva siku ya Jumapili, ili kuwashawishi baadae wakutane katika meza moja ya mazungumzo.
Mjumbe huyo amesema anatarajia mazungumzo hayo yatakayodumu kwa takriban siku tatu yataweza kufikia suluhisho la mapambano yanayoendelea nchini Yemen baina ya waasi wa kihouthi wa madhehebu ya kishia wanaoungwa mkono na Iran pamoja na vikosi yilivyo tiifu kwa rais aliyoko uhamishoni nchini Saudi Arabia Abd-Rabbu Mansour Hadi.
Ufunguzi wa mazungumzo hayo pia utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/RTREA/FPE/DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga