Waasi wa Kishia wakubali mazungumzo ya Geneva
5 Juni 2015Mazungumzo hayo ya Geneva yanalenga kuumaliza mgogoro uliodumu zaidi ya miezi miwili na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 2,000 nchini Yemen.
Mkutano huo wa Geneva, Uswisi, ambao umepangwa kuandaliwa Juni 14, utakuwa juhudi ya kwanza muhimu ya kusitisha mapigano ambayo yamesababisha kile Umoja wa Mataifa umekiita kuwa ni “janga” la kibinaadamu
Waasi wa Houthi wamesema wameitikia mwaliko wa Umoja wa Mataifa wa kukaa kwenye meza ya mazungumzo mjini Geneva bila masharti yoyote. Akizungumza na shirika la habari la AFP, Daifallah al-Shami, mwanachama wa tawi la kisiasa la waasi hao amesema hawatakubali masharti kutoka kwa pande nyingine za mazungumzo hayo.
Ezzedine al-Isbahi, waziri wa habari wa serikali ya Yemen iliyoko uhamishoni nchini Saudi Arabia, amesema pia itautuma ujumbe wake nchini Uswisi. Mazungumzo ya Geneva yatajaribu kufikia makubaliano ya kuweka chini silaha, makubaliano ya mpango wa wahouthi kuondoka katika maeneo ya vita, na kupelekwa misaada ya kiutu.
Mapema wiki hii, Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani wa masuala ya Mashariki ya Karibu Anne Patterson alikutana na wawakilishi wa Houthi nchini Oman ili kuwashawishi kushiriki mkutano wa Geneva. Patterson pia alikuwa Sauidi Arabia kwa mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo ya Kifalme pamoja na Rais wa Yemen Abderabo Mansour Hadi aliyekimbilia nchini humo mwezi Machi wakati waasi walipoingia katika mji wa bandari wa Aden ambao ulikuwa kama ngome yake.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Ould Cheick Ahmed alikutana na Hadi wiki hii baada ya kufanya mazungumzo katika mji mkuu wa Sanaa unaodhibitiwa na waasi. Mkutano wa Marekani na waasi, ambao wamesusia mazungumzo ya Riyadh na kusisitiza nchi isiyoegemea upande wowote, yalifuatia ujumbe wa wiki iliyopita wa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif mjini Muscat.
Oman ina mahusiano mazuri na Iran na Marekani, na aghalabu hutekeleza jukumu la upatanishi. Nchi hiyo ndio mwanachama pekee wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba lenye nchi sita wanachama, ambaye hajajiunga katika operesheni ya angani ya mashambulizi dhidi ya waasi wa houthi.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Josephat Charo