CORD walalamikia matokeo Kenya
6 Machi 2013Huku matokeo ya uchaguzi yakizidi kutiririka kutoka katika kituo cha kuhesabia kura jijini Nairobi, viongozi wa muungano wa CORD wamelalamika kwamba utaratibu unaotumiwa kutangaza matokeo hayo unatia shaka.
Kulingana na taarifa iliyosomwa na Kalonzo Musyoka, mgombea mwenza wa Raila Odinga, viongozi kutoka vyama vinavyounda muungano huo wameowaomba wafuasi wao kuwa watulivu wakati matokeo yote yanavyosubiriwa.
Kalonzo alisema kuwa bado wana uhakika wa kushinda katika uchaguzi na akaongeza kuwa endapo watashindwa wako tayari kusalimu amri.
Kauli ya CORD yanakuja wakati ambapo kinara wa mrengo wa Jubilee, Uhuru Kenyatta, anaonekana kuongoza katika matokeo ya awali yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Hata hivyo, Kenyatta na mpinzani wake wa karibu Odinga wanamenyana vilivyo huku kila mmoja wao akiwa ametimiza zaidi ya kura milioni mbili.
Katika mkutano na waandishi wa habari, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Bw. Isaack Hassan amewaomba wanasiasa wawe watulivu wakati huu wa kuhesabiwa kwa kura na akakiri kuwa kulikuwa na hitilafu Fulani za kimitambo ambazo zilichangia kucheleweshwa kwa matokeo.
Hata hivyo, mgombea mwenza wa muungano wa Jubilee, William Ruto, alisiifu IEBC kwa kuendeleza shughuli za uchaguzi kwa utaratibu unaofaa. Ruto amewashukuru Wakenya kwa kujitokeza kwa wingi ili kupiga kura siku ya Jumatatu.
COMESA, EAC watoa ripoti ya awali
Wakati huo huo, tume ya wangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na mataifa wanachama wa COMESA imetoa ripoti yao ya mwanzo kuhusiana na zoezi nzima la uchaguzi.
Kiongozi wa ujumbe huo, Abdulrahman Kinana kutoka Tanzania, amesema kuwa uchaguzi wa Kenya uliendeshwa kwa njia ya kidemokrasia na kuisifu tume ya uchaguzi kwa kutekeleza wajibu muhimu kulingana na katiba.
Hadi kufikia majira ya jioni, kura bado zilikuwa zikihesabiwa na matokeo kamili yanatarajiwa wakati wowote. Kwa mujibu wa katiba, tume inayo nafasi ya kutoa matokeo yote katika kipindi cha wiki nzima tokea siku ya kupiga kura.
Mwandishi: Reuben Kyama/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef