Kura zilizoharibika mtihani Kenya
6 Machi 2013Wasiwasi kutoka pande zote mbili za wagombea wakuu uko wazi, na hasa juu ya kiwango cha kura zilizoharibika, ambazo zinaweza kumuondosha Kenyatta kwenye nafasi ya kuongoza na hivyo kulazimika kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi hapo mwezi Aprili.
Kwa ujumla, hisabu ya kura imekuwa ikienda taratibu tangu ilipoanza siku ya Jumatatu, huku vifaa vipya vya kielektoniki vikikumbwa na matatizo na hivyo kusababisha vyama vya siasa kulalamika na wasiwasi kupanda miongoni mwa wapigakura wanaohofia kujirejea matukio ya miaka mitano nyuma, pale mgogoro wa matokeo ya kura ulipogeuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Hadi sasa, ikiwa robo moja ya kura imeshahisabiwa, Naibu Waziri Mkuu Kenyatta, anaongoza kwa asilimia 51 ya kura, ingawa nyingi ya kura hizo zinatoka kwenye ngome za Kenyatta, huku kura za maeneo mengi yanayomuunga mkono Waziri Mkuu Raila Odinga zikiwa bado hazijatangazwa.
Uchaguzi wa mwisho hapo mwaka 2007 ulishuhudia kiasi cha watu 1,200 wakiuawa kwenye ghasia za kikabila baada ya rais anayemaliza muda wake, Mwai Kibaki, kutangazwa mshindi dhidi ya Odinga huku kukiwa na tuhuma kadhaa za wizi wa kura.
Katika uchaguzi wa mara hii, tayari watu 15 wamesharipotiwa kuuawa katika matukio mbalimbali ya ghasia, ingawa tangu Jumatatu hali imeendelea kuwa shwari kwa takribani sehemu zote za nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki.
Mtihani mkubwa
Mtihani mkubwa, hata hivyo, ni iwapo viongozi wa kisiasa na wafuasi wao watayakubali matokeo kamili yatakapotangazwa na IEBC. Tume hiyo imesema kwamba ina matumaini kuwa itaweza kutoa matokeo kamili leo Jumatano (tarehe 6 Machi), ingawa kwa mujibu wa sheria ina hadi siku saba kutokea kura zilipopigwa kutangaza matokeo.
"Tunaogopa kwa sababu hatujui kitakachotokezea baadaye," alisema Charles Kabibi, kijana wa miaka 27 anayefanya kazi kama mtunza bustani kwenye bandari ya Mombasa, ambaye anasema kila kukicha hofu yake inazidi kuongezeka.
Kenyatta na mgombea wake mwenza, William Ruto, wanatakiwa mjini The Hague, Uholanzi, kukabiliana na mashitaka ya kusababisha mauaji baada ya uchaguzi wa mwaka 2007. Wote wawili wanakana mashitaka hayo.
Marekani na nchi nyengine za Magharibi, ambazo ni wafadhili wakubwa wanaoiona Kenya kama mshirika muhimu katika mapambano dhidi ya Waislamu wenye siasa kali, tayari zimeionya kwamba ushindi wa Kenyatta utayatia hatarini mahusiano ya kidiplomasia.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdulrahman