Congo kuanza kutumia chanjo ya pili ya majaribio ya Ebola
23 Septemba 2019Maafisa wakuu wa afya katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wamesema Jumamosi kwamba wanapanga kuanzisha chanjo ya pili ya ugonjwa wa Ebola iliyotengezwa na kampuni ya Johnson and Johnson kukabiliana na mkurupuko wa pili mbaya zaidi wa virusi vya ugonjwa huo katika historia.
Tangu mkurupuko wa ugonjwa wa Ebola kutangazwa mnamo mwezi Agosti mwaka jana, zaidi ya watu laki mbili wamepokea chanjo iliyotengezwa na kampuni ya Merck ambayo itaendelea kutumiwa nchini Congo. Katika taarifa, taasisi ya afya ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa chanjo hiyo ya pili iliyotengezwa na kampuni ya Johnson and Johnson itaanza kutumiwa mwezi Oktoba katika maeneo ambayo ugonjwa huo wa Ebola hauenei kwa haraka.
Kulingana na mkurugeni wa shirika la afya duniani katika eneo la Afrika Matshidiso Moeti, matumizi ya chanjo ya Johnson and Johnson yatakahakikisha kuweko kwa mbinu ya ziada ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo. Kufikia sasa, zaidi ya watu 3030 wameathirika kutokana na mripuko wa virusi vya ugonjwa wa Ebola, wa pili mbaya zaidi katika historia na wengine zaidi ya 1990 kufariki.
Swali la iwapo chanjo ya majaribio ya kampuni ya Johnson and Johnson inapaswa kutumiwa lilikuwa suala kuu katika mzozo kati ya aliyekuwa waziri wa afya wa Congo Dr. Oly Ilunga na maafisa wakuu wa afya ulimwenguni. Ilunga alikuwa amesisitiza kuwa Congo haitatumia chanjo hiyo kwa sababu haikufanyiwa uchunguzi makhsusi na itasababisha hali ya kutoeleweka.
Alijiuzulu kama waziri wa afya mwezi Julai baada ya rais kumpa majukumu mapya kama mkuu wa kundi linalokabiliana na ugonjwa wa Ebola. Mbali na hayo shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka inataka kubuniwe kamati huru ya kusimamia juhudi za chanjo ya ugonjwa wa Ebola sawa na zile zilizobuniwa kimataifa kushughulikia mkurupuko wa magonjwa kama utandu wa ubongo, homa ya njano na kipindupindu.
Shirika hilo linasema kuwa uwazi wa kiwango kikubwa unahitajika na kudai kuwa shirika la afya duniani linadhibiti kupatikana kwa chanjo ya Merck. Shirika hilo limeendelea kusema kuwa idadi ya takriban watu elfu 225 waliopata chanjo hiyo kufikia sasa haitoshi na kwamba watu kati ya elfu 450 na 600 wanapswa kuwa wamepata chanjo hiyo kufikia sasa.