Chanjo mpya ya Ebola kuanza kutumika Congo
21 Septemba 2019Maafisa wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wamesema wanapanga kuanza kuitumia chanjo ya pili ya Ebola iliyotengenezwa na kampuni ya Johnson&Johnson,ili kukabiliana na mripuko wa ugonjwa huo.
Timu inayofuatilia mapambano dhidi ya maradhi hayo nchini Kongo haijasema lini haswa chanjo hiyo itaanza kutumika. Chanjo hiyo itatumika kuchukuwa nafasi ya chanjo nyingine ya Ebola iliyotengenezwa na kampuni ya Merck iliyotumiwa kwa watu zaidi ya 225,000 tangu mwezi Agosti mwaka 2018.
Chanjo ya J&J imekuwa chanzo cha utata miongoni mwa maafisa wa afya nchini Kongo. Aliyekuwa waziri wa afya aliyefutwa kazi kutokana na sakata la madai ya kusimamia vibaya mapambano dhidi ya Ebola mwezi Julai anapinga matumizi ya chanjo hiyo akisema bado haijathibitishwa kuwa salama au kuwa na ufanisi.
Lakini kwenye taarifa yake, timu ya sasa ya kukabiliana na Ebola imesema chanjo hiyo ni salama na kugusia kwamba tayari imeshafanyiwa majaribio katika nchi jirani ya Uganda na Guinea huko Afrika Magharibi. Timu hiyo imehoji kwamba ni kwa nini chanjo iliyokwisha tumiwa na nchi jirani kwanini Congo isitumike kuulinda umma wake?
Katika taarifa hiyo maafisa wa afya wanalenga kuanza kuitowa chanjo hiyo ya J&J kwa wakongomani wafanyabiashara wanaovuka mpaka kuingia nchi za Rwanda pamoja na wakaazi wa mikoa inayopakana na kitovu cha mripuko huo ili kujenga mfumo wa kupambana na maradhi hayo miongoni mwa watu wa eneo hilo.
Mripuko huu mpya wa Ebola umeshaua zaidi ya watu 2,100 tangu katikati ya mwaka uliopita,ukiwa ni mripuko wa pili kwa ukubwa baada ya ule ulioshuhudiwa mwaka 2013 mpaka 2016 katika nchi za Afrika Magharibi ambapo watu 11,300 walifariki.
Mwandishi: Saumu Yusuf
Mhariri: Angela Mdungu