City waandika historia ya mataji manne ya ligi mfululizo
20 Mei 2024Pep Guardiola na jeshi lake la Manchester City waliandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kushinda ubingwa kwa msimu minne mfululizo. Waliwashinda wapinzani wao wa karibu Arsenalkatika kinyang'anyiro cha msimu huu na pengo la pointi mbili.
Soma pia: Ubingwa wa Ligi kuu ya England ni mbio za farasi wawili
Pep ametilia shaka mustakabali wake wa muda mrefu katika klabu ya City, akikiri kuwa inakuwa vigumu kupata motisha baada ya mafinikio mengi aliyoyapata kwa mfululizo. "Kwa hiyo, ni nini kinachofuata? Sijui sasa hivi. Lakini kitu kinachofuata ninachojua ni Kombe la FA (fainali dhidi ya Manchester United). Lakini msimu ujao, kwa sasa sijaweza kujua hasa motisha itakuwa nini kufanya hivyo kwa sababu ni vigumu wakati mwingine kuipata, wakati kila kitu kimeshatimizwa.”
Klopp aiaga Liverpool
Na mmoja wa watu ambao walikuwa wakimkosesha usingizi katika safari ya mafanikio hayo, amewaaga rasmi mashabiki baada ya miaka 9. Mjerumani Jurgen Klopp, aliwaliza mashabiki wa Liverpool, wachezaji na hata wafanyakazi katika dimba la Anfield baada ya kusimamia mechi yake ya mwisho waliyopata ushindi wa 2 – 0 dhidi ya Wolves na kumaliza katika nafasi ya tatu msimu huu. "Kazi imekamilika. Ninawapenda nyote na napenda kila kitu kuhusu klabu hii lakini ni wakati wa mimi kuondoka. Lakini sio kwamba kuna moto unaowaka nyuma yangu na hilo linanipa hisia nzuri. Sio kwamba natimuliwa hapa na kuambiwa ondoka! Kwa hivyo, najua ninaweza kurudi na nitarudi na jinsi nilivyosema baada ya mechi, kuanzia leo, kutoka saa tatu zilizopita wakati mchezo ulipomalizika, mimi ni mfuasi wa Liverpool na napenda hilo."
Klopp mwenye umri wa miaka 56, alijiunga na The Reds mwaka wa 2015 na kushinda mataji yakiwemo Ligi ya Mabingwa, na taji la kwanza la Ligi Kuu katika miongo mitatu. Mikoba ya Klopp inachukuliwa na Mholanzi Arne Slot ambaye aliiongoza Feyenoord kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Uholanzi msimu huu.
afp, ap, dpa, reuters