1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China yaliponda kundi la G7 kwa 'upotoshaji'

Daniel Gakuba
14 Juni 2021

Viongozi wa kundi la G7 wamemaliza mkutano wao kwa kuchapisha tangazo ambalo miongoni mwa mengine linaihimiza China iheshimu haki za binadamu na uhuru wa watu. China imesema hilo ni kuingilia mambo yake ya ndani.

https://p.dw.com/p/3urMt
Chinesische Flagge
Picha: Marko Beric/Zoonar/picture alliance

Katika tangazo la kuhitimisha mkutano wao uliofanyika nchini Uingereza, viongozi wa nchi hizo zinazounda kundi la G7 ambazo Marekani, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Italia, Canada na Japan wameikosoa China vikali zaidi kuliko walivyokuwa wakifanya siku za nyuma.

Soma zaidi: Viongozi wa G7 waahidi dozi bilioni 1 dhidi ya COVID-19 

Wamesema wako tayari kuiwajibisha China kwa mienendo yake ya kukiuka masharti ya kibiashara, kukanyaga haki za binadamu na kukandamiza uhuru katika mji wa Hong Kong ambao hadi 1997 ulikuwa koloni la Uingereza.

Eneo jingine ambalo kundi la G7 limeikosoa China ni kuhusu uhusiano na Taiwan, kisiwa chenye serikali yake ambacho China inasisitiza kuwa ni sehemu yake ambayo kamwe haiwezi kujitenga.

G7-Gipfel in St Ives 2021
Wakuu wa nchi za G7 kwenye meza ya mazungumzoPicha: Koji Ito/Yomiuri Shimbun/picture alliance

Canada yaongoza mashambulizi

Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau, nchi mojawapo yenye mivutano mikubwa na China, amesema ameridhishwa na muafaka uliofikiwa katika kukabiliana na utawala wa Beijing.

''Katika mkutano huu, Canada imeongoza njia juhudi za kupata makubaliano kuhusu namna ya kuikabili China. Kama washirika lazima tuwe imara na kuwa na umoja, na wikendi hii tumeafikiana jinsi ya kufikia azma hiyo.'' Amesema Trudeau.

China, kupitia ubalozi wake mjini London imetupilia mbali ukosoaji huo dhidi yake, ikisema ni uingiliaji katika masuala ya ndani na upotoshaji wa hali halisi ya mambo.

UK G7-Gipfel im Gartenanlage "Eden Project" in Cornwell
Rais Joe Biden wa Marekani (mbele) amerejesha hali ya uelewano katika kundi la G7 na jumuiya ya NATOPicha: Jack Hill/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa ubalozi huo amesema mkutano huu umedhihirisha hila ya Marekani na nchi nyingine chache, kujumuika katika makundi madogo madogo kwa nia ya kutimiza malengo yao ya kisiasa.

Hong Kongo na Taiwan ziko nje ya mjadala

Kuhusu Hong Kong, msemaji huyo wa ubalozi wa China mjini London amezitaka nchi za G7 kukubali ukweli kuwa mji huo wa kisiwa ni sehemu ya China, na kusisitiza kuwa chini ya sera ya China moja, Kisiwa cha Taiwan hakiwezi kamwe kutenganishwa na China.

Amekanusha pia shutuma za China kukiuka masharti ya biashara ya kimataifa, akiurudisha mpira wa lawama kwa Marekani aliyoituhumu kuyanyanyasa makampuni ya China kwa kisingizio cha usalama wa taifa.

Soma zaidi: China na Magharibi, washirika na washindani

Mvutano baina ya China na nchi za G7 ambazo zote isipokuwa Japan ni wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO, unahamia katika mkutano wa jumuiya hiyo ulioanza asubuhi ya leo mjini Brussels.

Rais wa Marekani Joe Biden anahudhuria mkutano huo, akiazimia kurejesha uelewano miongoni mwa wanachama wa NATO ambao ulivurugika chini ya uongozi mtangulizi wake, Donald Trump.

 

AFP, dpa, Reuters