1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Magharibi, washirika na washindani

9 Juni 2021

Mataifa ya Magharibi yamo kwenye mfumo wa ushindani na China changamoto za ulimwengu zinawalazimisha kuwa washirika zaidi kama Kongamano la Usalama la Munich inavyojaribu kutafuta uwiano wenye manufaa kwa pande zote.

https://p.dw.com/p/3uelo
China Tarnkappenbomber Guying J-31
Picha: picture-alliance/dpa/Li Jianshu

Wakati umechaguliwa vyema: Rais Joe Biden wa Marekani anaanza ziara yake barani Ulaya - kwanza kwenye mkutano wa kilele wa mataifa ya G7 nchini Uingereza, kisha mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO mjini Brussels. Viongozi wa mataifa ya muungano huo wenye nguvu kubwa kijeshi wanakutana kabla ya Biden kukutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi mjini Geneva. 

Katika mazingira kama hayo, ndipo Kongamano la Usalama la Munich linapochapisha ripoti yake mpya ya Usalama iliyopewa jina "Baina ya Hali za Uhasama – Ushindani na Ushirikiano".

Jina lenyewe tayari linaelezea kizungumkuti kikubwa kilichopo: serikali za Kimagharibi zinajihisi kuwa zinakabiliwa na changamoto kubwa, hasa kutoka China, lakini wakati huo huo zinahitajiana sio tu kama washirika wa kibiashara, bali pia kukabiliana na changamoto kubwa zaidi za kilimwengu. 

Mfano wa wazi kabisa ni janga la virusi vya corona, mabadiliko ya tabia nchi na ushindani wa silaha za nyuklia.

Kwa hivyo, licha ya yote mengine, China inaonekana kuwa ni mshirika rasmi wa kimkakati na mshindani wa Umoja wa Ulaya kwa wakati mmoja.

Uimara wa China

China ambayo inaongozwa na wakomunisti wanaoendesha nchi kwa ubepari wa dola imefanikiwa katika kile ambacho Umoja wa Kisovieti ulishindwa: mchanganyiko wa utawala wa kiimla na mafanikio ya kiuchumi na ukuwaji wa ustawi wa wananchi wao.

Brasilien Brasilia BRICS Treffen 16.07.2014 Xi Jinping
Rais Xi Jinping wa China.Picha: EDILSON RODRIGUES/AFP/Getty Images

Hii ndiyo sababu kwa nini kauli za kujilinda zinazosikika mara kwa mara kwenye hutuba za Joe Biden, kama mathalani pale anaposema: "Tunapaswa kuonesha kwamba serikali za kidemokrasia bado zinaweza kuwahudumia watu wetu vyema katika dunia inayobadilika."

Inaonekana kwamba ikiwa taifa lenye watu bilioni 1.4 linakuwa kiuchumi kwa kiwango cha tarakimu mbili kwa miaka miongo minne mfululizo, inamaanisha kuwa taifa hilo kuna wakati fulani linaweza kuitafsiri nguvu yake ya kiuchumi kuwa nguvu ya kisiasa – na bila ya shaka pia kuwa nguvu ya kijeshi.

Na Beijing imejiwekea malengo makubwa: kufikia maadhimisho ya miaka 100 tangu kuundwa kwa Jamhuri ya Watu hapo mwaka 2049, China inataka kuwa taifa lenye nguvu na la kisasa la kisoshalisti, inataka iwe na uwezo wa kuweka na kuunda kanuni  na kuwa na kiwango cha juu cha teknolojia, uchumi na utamaduni. Maana yake kuwa taifa linaloongoza Dunia.

Ripoti hiyo ya Usalama ya Munich inaeleza kwamba wawakilishi wa demokrasia za kiliberali sasa wanataka kujilinda dhidi ya ushindani usio wa kiliberali.

Kama anavyosema Tobias Bunde, mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo na ambaye pia Mkurugenzi wa Utafiti wa Kongamano la Usalama la Munich akimnukuu Joe Biden kwenye utangulizi wa ripoti yenyewe: "Tupo kwenye njia panda na serikali za kidemokrasia ulimwenguni lazima ziungane pamoja."