China inajaribu kuigeuza Taiwan kuwa 'Hong Kong'.
11 Agosti 2020Taiwan imetoa onyo hili kwenye ziara ya kihistoria na ya kidiplomasia ya waziri wa afya wa Marekani Alex Azar mjini Taipei. Ziara hiyo hata hivyo inakosolewa vikali na China, ambayo inadai Taiwan ni sehemu ya milki yake.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Taiwan Joseph Wu amemwambia waziri huyo wa afya wa Marekani, Azar kwamba Taiwan inakabiliwa na vitisho vya mara kwa mara dhidi ya uhuru wake. Amesema maisha ya kila siku ya watu wa Taiwan yamekuwa magumu zaidi wakati China ikiendelea kuishinikiza Taiwan kukubaliana na masharti yake ya kisiasa, hali ambayo huenda ikaibadilisha Taiwan kuwa Hong Kong inayokuja.
Hatua kali dhidi ya wakosoaji wa China katika jiji la kibiashara la Hong Kong zimeongezeka tangu ilipoanzisha sheria mpya na pana ya usalama mwezi Juni, huku wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wakikamatwa.
Kuongezeka kwa hatua hizo kali kumeishtusha Taiwan, inayojitawala na yenye idadi ya watu milioni 23 ambayo Beijing inadai kuwa ni eneo lake na kuapa kulichukua hata kwa kutumia nguvu, iwapo italazimika kufanya hivyo.
Waziri Azar yuko Taipei kwa ziara ya siku tatu na inayochukuliwa kama ya ngazi za juu kabisa kutoka Marekani katika kipindi cha miongo minne. Ziara yake hiyo inakuja katika wakati ambapo mahusiano kati ya Marekani na China yakiwa yanatokota kufuatia mivutano kuanzia ya kibiashara, kijeshi, masuala ya usalama hadi janga la virusi vya corona.
Mnamo siku ya Jumatatu, Taiwan ilisema China imepeleka ndege za kijeshi katika eneo tete la mpaka na linalowatenganisha mahasimu hao wawili muda mfupi tu kabla Azar hajakutana na rais wa Taiwan Tsai Ing-wen hatua ambayo Taiwan inaiona kama ilikuwa ni udhalilishaji dhidi yake.
China imependekeza mfumo wa utawala wa taifa moja, mifumo miwili ili kuishinikiza Taiwan kukubaliana na utawala wake kama ule ambao inautumia kwa Hong Kong. Pendekezo hilo limekataliwa na vyama vyote vikubwa vya siasa pamoja na serikali ya Taiwan.
Wu amesema, Taiwan ina bahati ya kuwa na marafiki kama Azar nchini Marekani anayeweza kuwasaidia kupambana katika masuala ya kimataifa. Alisema wanatambua suala hilo halihusiani tu na hadhi ya Taiwan lakini ni kuhusu uendelezwaji wa demokrasia dhidi ya uvamizi wa kibabe. Akasema, Taiwan ni lazima ishinde na demokrasia ichukue mkondo.
Washington, ilivunja mahusiano rasmi na Taipei mwaka 1979. Serikali ya Trump hata hivyo imeendelea kutoa kipaumbele katika suala la kuimarisha mahusiano na kisiwa hicho, wakati urafiki na China ukizidi kuzorota.
Azar yuko Taiwan kutoa sio tu msaada wa kiutawala, lakini pia kujifunza kuhusu mafanikio ya taifa hilo katika mapmbano dhidi ya virusi vya corona. Taiwan imesalia na idadi ya chini kabisa ya maambukizi, na hasa kutokana na hatua zake ya mwanzoni kabisa za kudhibiti maambukizi.
Aidha kwenye ziara hiyo, Azar alisifu demokrasia ambayo Taiwan inaionyesha pamoja na mafanikio yake katika vita dhidi ya janga la COVID-19. Awali alikosoa namna ambavyo Beijing inalishughulikia janga hilo lililoanzia katikati ya nchi hiyo, lakini pia akikosoa utawala wa kiimla wa serikali ya Beijing.
Soma Zaidi: Virusi vya Corona: Yote unayopaswa kujua
Mashirika: AFPE/RTRE