1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Virusi vya Coronav: Yote unayopaswa kujua

Zainab Aziz Mhariri:Iddi Ssessanga
28 Januari 2020

Watu zaidi ya mia moja wameshakufa kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona nchini China na maalfu wengine wameambukizwa. Je dalili zake ni zipi? na jee virusi hivyo vinaambukizaje?

https://p.dw.com/p/3Wvwe
Symbolbild Saudi-Arabien Krankenhaus
Picha: BEHROUZ MEHRI/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa taarifa ya madakatari wa China maambukizi ya virusi vipya vya Corona yanaweza kutokea kati ya mtu na mtu na kwamba virusi hivyo vina uwezo wa kujibadilisha hali inayoweza kusababisha kuenea haraka na kufanya iwe vigumu kutibika.

Hatua gani zinaweza kuchukuliwa ili kuepusha maambukizi?

Mpaka sasa kasi ya maambukizi ya virusi hivyo haijabainishwa, ingawa inafahamika kwamba watu huambukizwa aina nyingine ya virusi hivyo kwa njia ya kikohozi na kuchemua lakini pia bado haijathibitishwa iwapo vijidudu hivyo vinaambukizwa kwa kupitianjia ya mfumo wa kupumua.

Mkasa wa kwanza ulibainika kwenye mji wa Wuhan nchini China, na baada kufuatilia iligundulika kwamba virusi hivyo vimetokea kwenye soko la nyama na samaki. Soko hilo sasa limefungwa. Yumkini maambukizi yalikuwa kati ya binadamu na binadamu moja kwa moja au yalitokea kwa njia yavijidudu kupeperushwa na hewa kama ilivyo kawaida kwa maradhi mengine.

Mtu anawezaje kujua iwapo ameambukizwa virusi vya Corona?

Dalili zake zinaonekana katika kukohoa, kupumua kwa taabu na kupata homa. Vijidudu hivyo pia vinaweza kusababisha maradhi ya kichomi yaani uvimbe kwenye mapafu unaosababisha usaha.

Virusi vya Corona vimeripotiwa pia nchini Thailand, Japan, Korea Kusini,Taiwan na Marekani. Wataalamu wamefanikiwa kuvichambua vinasaba vya Corona. Virusi hivyo viligundulika mnamo miaka ya 60. Kwa mujibu wa wataalamu virusi hivyo si vya hatari kubwa lakini vina uwezo wa kubadilika ndiyo kusema vinaweza kuenea haraka na kuwaambukiza viumbe mbalimbali na kusababisha vifo.

Vipi mtu anaweza kuepuka maambukizi?

Jambo la kwanza ni kuzingatia ni usafi wakati wote. Pili inapasa kuepuka kukaribiana na watu wenye mafua na vikohozi vikali na pia inashauriwa kuepueka wanyama pori waliohai au waliokufa. Mtu anapaswa kunawa mikono kila mara na hasa baada ya kukaribiana na mtu mwenye maambukizi. Hata hivyo wataalamu hawatarajii kuenea kwa maambukizi ya Corona duniani kote.

Wataalamu nchini Ujerumani wamesema hakuna haja ya kuchukua tahadhari maalumu nchini humo. Wamesema hatari siyo kubwa lakini wameshauri kwamba inapasa kuwa macho. Wakati huo huo masoko ya hisa barani Asia, yameanguka kutokana na wasi wasi uliosababishwa na mlipuko wa virusi vya corona. Wafanyabiasha  bado wanakumbuka athari za kiuchumi zilizosababishwa na ugonjwa wa homa ya ndege uliozuka kuanzia mwaka 2002  hadi 2003. Sekta za utalii na usafirishaji zinaweza kuathirika na kutokana na watu kuibana mifuko yao. 

Vyanzo:https://p.dw.com/p/3WcEg/AP