Chama cha AKP chashinda uchaguzi wa Uturuki
2 Novemba 2015Akizungumza leo na waandishi wa habari kwenye msikiti mjini Istanbul, Rais Erdogan amesema Waturuki wamepiga kura kwa ajili ya utulivu, baada ya chama chake cha AKP, kushindwa kuendelea kushikilia viti vingi bungeni katika uchaguzi wa mwezi Juni.
Amesema Waturuki wameonyesha ushahidi tosha kwamba wana shauku kubwa kuhusu umoja na uadilifu wa nchi yao, hali iliyochangia kukirejeshea chama chake wingi wa viti bungeni.
Televisheni ya taifa ya Uturuki, imetangaza kuwa chama cha AKP, kilichoanzishwa na Rais Erdogan mwaka 2001, kimeshinda kwa zaidi ya asilimia 49 ya kura na kilikuwa kinatarajiwa kupata viti 316 vya bunge.
Matokeo ya awali yametangazwa baada ya asilimia 99 ya kura kuhesabiwa, hivyo kukipa chama hicho wingi wa viti kwenye bunge hilo lenye jumla ya viti 550.
Uchaguzi uliitishwa mapema
Uchaguzi huo wa bunge ulioitishwa mapema, umeirejesha Uturuki katika serikali ya chama kimoja, miezi mitano tu baada ya kuupoteza utawala huo kutokana na ushindani mkali wa chama cha mrengo wa kushoto kinachowaunga mkono Wakurdi cha HDP, ambacho kwenye uchaguzi wa jana kimepata zaidi ya asilimia 10 ya kura zilizopigwa.
Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, amesema huo ni ushindi mkubwa kwao. Akizungumza kwenye makao makuu ya chama hicho, amewataka Waturuki kuendelea kubakia watulivu. Aidha, Davutoglu ametoa wito kwa vyama vya kisiasa kuungana pamoja na kukubaliana kuhusu kuunda katiba mpya.
''Ninavisihi vyama vyote vilivyoingia bungeni kuunda katiba mpya kwa maslahi ya nchi, mfumo wa uchaguzi unaoaminika, serikali ya uwazi na siasa zisizo na urasimu. Tufanye kazi kwa pamoja kwa ajili ya katiba huru na mabadiliko ya baada ya mapinduzi ya katiba, alisisitiza Davutoglu.''
Davutoglu amesema chama chake cha AKP, kitaongoza kwa maslahi ya Waturuki wote. Nacho chama cha mrengo wa kati cha CHP, kimepata asilimia 25 ya kura ambazo ni sawa na zile ilizopata katika uchaguzi wa mwezi Juni, na hivyo kushika nafasi ya pili. Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa ndani ya siku 12 zijazo.
Wakati huo huo, katika eneo la kusini-mashariki mwa Uturuki, polisi walipambana na waandamanaji wa Kikurdi waliokuwa wakiyapinga matokeo hayo, wakisema uchaguzi haukuwa wa haki. Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi, huku waandamanaji wakiwarushia mawe polisi. Nao wafuasi wa HDP mjini Berlin wameelezea kusikitishwa na matokeo hayo yaliyokipa ushindi chama cha AKP.
Aidha, sarafu ya Uturuki, Lira leo imeimarika dhidi ya Dola ya Marekani, baada ya chama cha AKP kurejea madarakani.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ RTRE, AFPE, DPAE, APE
Mhariri:Josephat Charo