Uchaguzi wa mapema huenda ukaitshwa
13 Agosti 2015Afisa mmoja wa chama cha upinzani CHP ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa mkutano uliodumu kwa saa moja na nusu mjini Ankara kati ya Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmeti Davutoglu na kiongozi wa CHP Kemal Kilicdaroglu umekamilika bila muafaka wowote. Mkutano huo umekuja baada ya wiki kadhaa za mazungumzo baina ya vyama hivyo viwili.
Afisa huyo hajatoa maelezo zaidi, lakini Davutoglu na chama cha CHP wanatarajiwa kutoa taarifa zao tofauti hapo baadaye. Uturuki haijawa na serikali kamili tangu chama tawala cha Haki na Maendeleo – AK kilipopoteza wingi wake wa viti katika uchaguzi wa bunge wa Juni 7 kwa mara ya kwanza tangu kilipoingia madarakani mwaka wa 2002.
Mkwamo huo wa kisiasa unakuja wakati serikali ya Uturuki ikiendelea na mojawapo ya operesheni zake kubwa kabisa za usalama katika kipindi cha miaka mingi – mashambulizi ya mpakani dhidi ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu – IS na operesheni dhidi ya waasi wa chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi – PKK kaskazini mwa Iraq na kusini mashariki mwa Uturuki.
Wakati duru ya mwanzo ya mazungumzo ilianza vyema, wanasiasa wa upinzani na wachambuzi wamemshutumu Rais Recep Tayyip Erdogan kwa kuingilia kati mchakato huo ili kuchochea kuandaliwa uchaguzi wa mapema.
Hapo jana, Erdogan alidokeza kuwa hawezi kusumbuliwa na kushindwa kwa mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano, akisema kuwa kuvunjika kwa mazungumzo hayo hakutakuwa sababu ya kiongozi wa chama “kujitia kitanzi”.
Kwa mujibu wa katiba, Davutoglu – kama kiongozi wa chama kikubwa kabisa – ana hadi Agosti 23 kukubaliana kuhusu serikali ya muungano. Chama cha AK sasa kinatarajiwa kuandaa mazungumzo na chama cha upinzani cha uzalendo cha MHP, ambacho kimeashiria kuwa huenda kikaiunga mkono serikali ya AKP katika kipindi kifupi ikiwa itaandaa uchaguzi mpya.
Lakini afisa wa ngazi ya juu wa chama cha AK ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa nafasi za kuunda serikali ya muungano na chama cha MHP ni finyu sana. Amesema uwezekano wa kuandaliwa uchaguzi wa mapema mwezi Novemba upo juu mno kwa sasa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga