1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ugiriki kuupigia kura mpango wa kubana matumizi

29 Juni 2011

Licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi, bunge la Ugiriki linatarajiwa leo (29.06.2011) kuupitisha mpango wenye utata wa kubana matumizi unaopigiwa debe na Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

https://p.dw.com/p/11lQe
Muandamanaji wa Ugiriki akitumia mashine ya kuzimia moto dhidi ya polisi.
Muandamanaji wa Ugiriki akitumia mashine ya kuzimia moto dhidi ya polisi.Picha: ap

Wabunge wawili wa chama tawala cha Kisoshalisti (PASOK) wameonesha wasiwasi wao juu ya mswaada wa kukaza mkaja unaowasilishwa leo bungeni na serikali yao.

Alexandros Athanasiadis amesema ataupigia kura ya kuupinga, lakini mwenzake, Panayiotis Kouroumblis, hana uhakika wa nini atakifanya masaa machache yajayo.

Lakini wote wawili wanakiri kwamba, hata bila ya kura zao, mswaada huu utapita tu.

Nje ya bunge, wananchi wameendelea kujimwaga mitaani kuupinga mpango huu, wanaouona kwamba ni kitanzi cha kuwanyonga.

Wagiriki wengi wanaona kuwa wamesalitiwa na wanasiasa walioko serikalini na bungeni, na ndio sababu wakaamua kuingia mitaani kuonesha hasira zao.

"Haya ni mapambano dhidi ya sera zote za serikali ambazo hazina huruma kwa watu, sera ambazo zinashambulia pato la familia zenye mishahara midogo. Katika mgumo wa mipango ya muda wa kati, sera hizo zinazivuruga haki za tabaka zima la wafanyakazi." Amesema muandamanaji mmoja.

Waandamanaji wa Ugiriki mbele ya bunge la nchi yao wakijaribu kuzuia mswaada wa kubana matumizi.
Waandamanaji wa Ugiriki mbele ya bunge la nchi yao wakijaribu kuzuia mswaada wa kubana matumizi.Picha: dapd

Vyama vya wafanyakazi viliitisha mgomo wa kitaifa wa masaa 48 kuanzia hapo jana, ukiwa ni wa kwanza wa aina yake, kuishinikiza serikali isiupeleke mswaada huu bungeni na bunge lisiupitishe kama ukipelekwa.

Mgomo huu umeambatana na machafuko ya hapa na pale, ingawa hakuna taarifa za vifo hadi sasa. Katika mji mkuu wa Athens, hadi usiku wa manane, vijana waliendelea kukabiliana na polisi wa kuzuia fujo, huku vijana wakitumia mawe na fimbo na polisi wakitumia mabomu ya machozi.

Vyama vya wafanyakazi vimetishia kuwazuia wabunge kuingia kwenye jengo la bunge, lakini wachambuzi wanasema kwamba kitisho hiki kina fursa ndogo kabisa ya kuzuia mswaada wa kubana matumizi usijadiliwe na kupitishwa leo hii.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na wa Shirika la Fedha la Kimataifa wanasema kwamba ni lazima Ugiriki iupitishe mpango huu wa kubana matumizi, ikiwa inataka ipokee euro bilioni 12 zilizobakia kufufua uchumi wake.

Afisa wa ngazi ya juu anayehusika na uchumi kwenye Umoja wa Ulaya, Olli Rehn, amesema kuwa Ugiriki haina njia mbadala kwa sasa.

"Njia pekee ya kuepuka kushindwa kulipa deni kwa wakati, ni kwa bunge kuupitisha mpango huu wa kiuchumi. Ni lazima uidhinishwe ikiwa wanataka kupasa sehemu nyengine ya fedha. Hakuna Mpango B wa kuepuka kulipa deni." Amesema Rehn.

Wakati huo huo, taarifa kutoka Vienna, Austria, zinasema kuwa Jumuiya ya Nchi Zinazosafirisha Mafuta Duniani (OPEC) limepandisha bei ya mafuta kwa dola 2.03 zaidi za Kimarekani, muda mchache tu kabla ya bunge la Ugiriki kujadili mpango wa kubana matumizi.

Bei ya pipa moja la mafuta sasa imekuwa dola 103.59. Wachambuzi wa masuala ya fedha, wanasema kuwa bei hii ilipandishwa kwa matarajio kwamba wabunge wa Ugiriki wataupitisha mswaada huu.

Inahofiwa kwamba bila ya kupokea kiasi hiki cha fedha, Ugiriki itafilisika ndani ya wiki chache zijazo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPAE/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman