Buhari asifu ustadi wa kiutawala wa Jonathan
1 Aprili 2015Tume huru ya uchaguzi ya Nigeria ilitangaza kuwa Buhari mwenye umri wa miaka 72 na matawala wa zamani wa kijeshi alimshinda Jonathan katika uchaguzi huo uliyofanyika siku ya Jumamosi kwa tafauti ya kura milioni 2.6.
Buhari ameuelezea ushindi wake - ambao ni wa kwanza kwa mgombea wa upinzani tangu taifa hilo lenye wakaazi wengi zaidi barani Afrika kurejea kwenye mkondo wa demokrasia mwaka 1999, kama wa kihistoria. Amesifu ustadi wa kiutawala wa Jonathan kwa kukubali kushindwa katika kura hiyo iliyoshuhudia rais alieko madarakani akishindwa kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo.
"Majira ya saa 11 na robo kamili jana jioni, rais Goodluck Jonathan alinipigia simu kunipongeza juu ya ushindi wangu. Kwa hili nawaomba Wanigeria wote waungane nami kumpongeza na kumtambua Mheshiwa rais kwa ustadi wake wa kiutawala," alisema Jenerali huyo katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari baada ya kutangazwa kwa matokeo rasmi.
"Rais Joanathan ameendesha kampeni kali na alikuwa mpinzani anaestahili. Nampa mkono wa pongezi. Namhakikishia uelewa, ushirikiano na heshima kutoka kwa timu yangu na mimi, na watu wazuri wa Nigeria," aliongeza Buhari.
Jenerali Buhari ambaye aliingia madarakani kwa mara ya kwanza kupitia mapinduzi ya kijeshi miongo mitatu iliyopita, aliendesha kampeni yake kama mwana-demokrati alieokoka, akinuwia kuisafisha Nigeria kutokana na rushwa iliyokithiri. Tafauti ya kura, ambapo Buhari alipata kura milioni 15.4 dhidi ya kura milioni 13.3 za Jonathan, ilikuwa inatosha kuzuwia upinzani wowote dhidi ya ushindi wake.
'Nimetimiza ahadi yangu'
Akilihutubia taifa mapema Jumatano, rais Jonathan amewashukuru Wanigeria kwa muda wake aliokaa madarakani na kuongeza kuwa ametimiza ahadi yake ya uchaguzi huru na wa haki, akimtakia mema rais mteule na kuwataka wanachama wa chama chake kujivunia mafanikio yao badala ya kuhuzunika.
"Kwa wenzangu ndani ya chama cha People's Democratic Party PDP, nawashukuru kwa kuniunga mkono. Leo hii PDP inapaswa kusherehekea kuliko kuhuzunika. Tumeacha urithi wa uhuru wa demokrasia, uwazi, ukuaji wa kiuchumi na uchaguzi huru na wa haki. Kwa miaka 16 tumeiongoza nchi hii kutoka kwenye siasa za ukabila na udini," alisema Jonathan.
Rais Jonathan alisema waliiunda chama cha siasa kinachowajumlisha Wanigeria wote na kuwaletea watu maendeleo ya kiuchumi na mageuzi ya kijamii. Kupitia uzalendo na bidii, alisema wamejenga chama kikubwa zaidi na cha kizalendo katika historia historia ya Nigeria, na kuwataka waungane kama chama na kuuangalia wakati ujao kwa matumaini.
Mchakato wapongezwa
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosana Dlamini-Zuma amempongeza rais mteule Muhammadu Buhari, na kumsifu rais Jonathan kwa kukubali matokeo kwa wema. Katika taarifa yakeiliytolewa katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, Dlamini-Zuma alisema mataokeo ya uchaguzi huo yalibainisha ukomavu wa demokrasia nchini Nigeria.
Nayo Uingereza imesifu namna uchaguzi huo katika koloni laka la zamani ulivyoendeshwa na taarifa ya waziri wa mambo ya kigeni Philip Hammond imevitolea mwito vyama viwili vikuu, All Progressives Congress- APC cha Buhari na Peoples Democratic Party-PDP cha Jonathan kuhakikisha kuwa utaratibu wa kukabidhiana madaraka unafanyika kwa amani. Kwa mujibu wa Sheria, rais Jonathan atamkabidhi madaraka rais Mteule tarehe 29 mwezi Mei.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpae,ap,rtre.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman