Buhari ajitangaza mshindi Nigeria
31 Machi 2015Matokea ya mwanzo pia yanaonyesha mgombea huyo anaongoza dhidi ya rais wa sasa Goodluck Jonathan.Msemaji wa chama cha APC Lai Mohammed ameliambia shirika la habari la Reuters akiwa nyumbani katika mji mkuu Abuja ambako kiongozi wa chama Mohammadu Buhari anayafuatilizia matokea kwamba hii ni mara ya kwanza kabisa nchini Nigeria serikali iliyopo madarakani itaondolewa katika nafasi hiyo kupitia njia za wazi za kidemokrasia.
Ameongeza kusema kwamba chama chao hakina sababu ya kutilia shaka kwamba rais Goodluck Jonathan atakubali kushindwa.Vyombo vya habari nchini humo vinaripoti kwamba Mohamadu Buhari anaongoza katika matokeo hayo ya uchaguzi wa rais katika wakati ambapo tayari kura zimeshahesabiwa katika majimbo 25 kati ya 36 ambapo Buhari anatajwa kunyakua ushindi wa majimbo 13 na rais Jonathan akitwaa ushindi katika majimbo 12 ikiwemo mji mkuu Abuja.
Matokea hayo yamethibitishwa pia na tume ya uchaguzi iliyosema kwamba Buhari anaongoza kwa kiasi kura nusu milioni huku matokeo ya majimbo mengine 11 yakitarajiwa baadae leo jioni hii.Hata hivyo chama cha rais Jonathan cha People Democratic PDP kilionekana kutoridhika wakati tume ya uchaguzi ikitangaza baadhi ya matokeo mchana wa leo hali iliyozusha mtafaruku na mjibizano katika ukumbi wa kutangaza matokeo.Peter Godsday Orubebe ni mjumbe anaewakilisha chama hicho katika ukumbi huo na pia ni waziri wa zamani wa Niger Delta alisikika akimtuhu mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi Atahiru Jega kwa kuwa na upendeleo.
Lakini tuhuma hizo zilijibiwa na mkuu huyo wa Tume ya Uchaguzi Attahiru Jega aliyesema kila mmoja anwajibika kuwa muangalifu na matamshi anayotowa kueleka mchakato huo ulioanza kwa amani na ambao unatarajiwa kukamilika muda wowote kutoka sasa.
Pamoja na hayo chama cha rais Jonathan cha PDP na kile cha mpinzani wake Buhari vinatajwa kwamba ndivyo vitakavyonyakua viti vingi zaidi vya bunge la nchi hiyo lenye idadi jumla ya viti 360. Kutokana na hali ilivyo wakati matokeo rasmi kutoka tume ya uxchaguzi yakiendelea kusubiriwa kwa shauku kubwa maafisa kwenye majimbo wameshatangaza amri ya watu kutotembea usiku ingawa polisi wamesema hawana taarifa juu ya kutangazwa kwa hatua hiyo.
Ikumbukwe kwamba ili mgombea kushinda urais nchini humo anahitaji zaidi ya nusu ya idadi jumla ya kura kitaifa na alau asilimia 25 ya kura za thuluthi mbili ya majimbo yote 36 ya nchi.Endapo hakuna mgombea atakaeshinda moja kwa moja kwa wingi huo wa kura katika duru hii ya mwanzo uchaguzi utarudiwa ambapo mgombea anaweza kushinda kwa wingi mdogo wa kura.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman