1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS : Mawaziri wa mazingira wa Ulaya wakutana

20 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCQC

Mawaziri wa mazingira wa Umoja wa Ulaya leo hii wanatazamiwa kuunga mkono mipango ya kupunguza kwa kiwango kikubwa utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira wakati chama cha ulinzi wa mazingira duniani Greenpeace kikisisitiza kwamba Ulaya ina wajibu wa uadilifu kuongoza mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Mawaziri hao wanaokutana mjini Brussels wanatarajiwa kupigia kura mipango ya kupunguza gesi za carbon dioxide angalau kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2020 na hata ikiwezekana asilimia 30 kwa sharti kwamba nchi nyengine zilizoendelea zitakuwa tayari kuchukuwa hatua kama hiyo.

Ahadi hiyo itakuwa kanuni kuu ya mkakati wa Umoja wa Ulaya katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa baada ya mwaka 2012 wakati muda wa viwango vya sasa vya utowaji wa gesi hizo vilivyowekwa na Itifaki ya Kyoto utakapokuwa umemalizika.