1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter achungulia ushindi mwingine FIFA

Admin.WagnerD29 Mei 2015

Rais wa FIFA Sepp Blatter, amesema anaweza kutatua matatizo yanayoukabili mchezo wa soka ikiwa atachaguliwa tena kuwa rais wa shirikisho hilo, baada ya kukamatwa kwa maafisa wa juu wa soka wiki hii kuibua tafrani.

https://p.dw.com/p/1FYgR
Zürich FIFA Kongress Rede Sepp Blatter
Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Blatter anakabiliana na mpinzani mmoja katika kinyanganyiro hicho, mwanamfalme Ali bin Al-Hussain kutoka Jordan, lakini dalili zinaonyesha kiongozi huyo wa FIFA kwa miaka 17 sasa anaweza kushinda tena, licha ya kukaabiliwa na kashfa na mashinikizo kutoka Ulaya na Marekani.

Akiwahutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa FIFA unaofanyika nchini Uswisi, ambako wanachama watapiga Ijumaa kuamua juu ya urais wa shirikisho hilo la kandanda duniani, Blatter amewahimiza wanachama kuendelea kuwa na umoja.

"Matukio ya Jumatano yamesababisha mgogoro, na ilifika wakati masauli yakaanza kuulizwa ikiwa mkutano huu utafanyika au ajenga ingebadilishwa. Leo nakuombeni tuwe kitu kimoja ili tuweza kusonga mbele pamoja. Inaweza isiwe rahisi kila wakati lakini ni kwa sababu hii tuko hapa leo ili kushughulikia matatizo ambayo tumeyatengeneza. Tuko hapa kuyatatua," alisema Blatter.

Rais wa UEFA Michel Platini amesema Ulaya huenda ikasusia kombe la Dunia.
Rais wa UEFA Michel Platini amesema Ulaya huenda ikasusia kombe la Dunia.Picha: Reuters/R. Sprich

Wanachama 209 wa FIFA wataamua Ijumaa iwapo wanabakia na Blatter mwenye umri wa miaka 79, au kuhitimisha utawala wake wa miaka 17 kwa kumuunga mkono Mwanamfalme Hussain, ambaye anapigiwa upatu na shirikisho la kandanda la Ulaya UEFA, ambalo rais wake Michel Platini alimtaka Blatter mara mbili siku ya Alhamisi ajiuzulu bila mafanikio.

Nguvu ya Blatter bado ni kubwa

Lakini bado haijawa wazi iwapo mwanamfalme Hussain anawezakukusanya wingi wa kura 105 kati ya 209 wakati ambapo Blatter anaendelea kuwa maarufu hata baada ya miaka 17 usukani, huku mashirikisho ya Asia na Afrika yakiahidi kumuunga mkono Mswisi huyo katika hatua inayoweza kumhakikishia kura 100.

Sheikh Ahmed Al-Fahad Al-Sabah, anaeliwakilisha shirikisho la kandanda barani Asia kwenye FIFA na moja wa watu wenye nguvu zaidi katika mchezo wa soka duniani, alisema katika mahojiano siku ya Alhamisi kuwa Blatter ndiye mtu sahihi wa kuiongoza FIFA, na kushtumu kile alichokiita kutafuta kasoro za Blatter na kusahau mema yake.

"Tukipafuata mabaya na mazuri, nadhani bado ana mazuri mengi. Utulivu wa mchezo huu ni muhimu sana, na nadhani anaweza kuuendeleza utulivu huo. Kwa hilo sioni mgombea yeyote mwingine anaeweza kuchukuwa uongozi katika uchaguzi huu," alisema rais huyo wa Kuwait katika mahojiano.

Sheikh Ahmad Al Fahad Al Saba asema hakuna kama Blatter bado.
Sheikh Ahmad Al Fahad Al Saba asema hakuna kama Blatter bado.Picha: picture-alliance/AP Photo/Sakchai Lalit

Ulaya yatishia kususia kombe la dunia

Rais wa UEFA Michel Platini anasema laazima Blatter aondoke ili kuweza kuisafisha FIFA, na kuonya kuwa mataifa ya Ulaya yanaweza kususia mashindano ya kombe la dunia ikiwa hakutakuwa na mabadiliko ya rais.

Lakini wakati shinikizo likionekana kuzidi kwa Blatter kutoka kona mbali za dunia, ameonyesha kuwa kuwa mtu anaeweza kuhimili vishindo vya kashfa. Urais wake ulionekana kufikia tamani baada tu ya miaka minne wakati wakuelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2002, alipotuhumiwa kwa usimamizi mbaya wa fedha na kamati ya uongozi ya FIFA na malalamiko ya jinai kufunguliwa dhidi yake na waendesha mashtaka wa Uswisi. Lakini Blatter bado alimshinda Issa Hayatou, ambaye kwa sasa ni makamu wa rais wa FIFA.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,dpae,rtre,afpe
Mhariri: Saumu Yusuf